Skip to main content

KM asisitiza ulazima wa kudhibiti pamoja mabadiliko ya hali ya hewa duniani

KM asisitiza ulazima wa kudhibiti pamoja mabadiliko ya hali ya hewa duniani

Ijumanne adhuhuri KM Ban Ki-moon, alikutana na waandishi habari wa kimataifa waliopo Makao Makuu, na aliwaelezea kuhusu safari yake ya karibuni ambapo alitembelea yale maeneo yenye mizozo; na alizungumzia pia juu ya anuwai ya masuala yenye kukabili usalama na amani ya kimataifa.

Alitilia mkazo kwenye risala ya ufunguzi kwa waandishi habari, juu ya ulazima wa Mataifa Wanachama kushirikiana kwenye juhudi zao za kudhibiti pamoja matatizo yanayotokana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa katika dunia, suala ambalo, alisisitiza, ndilo aliolipa uzito mkuu, na ni mada ambaye alisema ilimhamasisha yeye binafsi, kuamua kuhudhuria Mkutano wa Uchumi wa Dunia wa Davos, uliofanyika majuzi Uswiss. Alipokuwepo Davos KM alipata fursa ya kuwahimiza wawakilishi wa kimataifa kupania vilivyo kulishughulikia suala la mabadiliko ya hali ya hewa kidharura, kwa masilahi ya umma wote wa dunia. Alisema ni muhimu kuyakamilisha majadiliano yajayo ya kimataifa ya kubuni Mkataba mpya wa kudhibiti bora mabadiliko ya hali ya hewa katika dunia, kama ifuatavyo:

"Majadiliano kuhusu Mkataba mpya wa kudhibiti athari za

mabadiliko ya hali ya hewa ulimwenguni, utakaofanyika mjini

Copenhagen, mwisho wa mwaka huu, yanahitajia uongozi wa kimataifa wa hali ya juu kabisa." KM alikumbusha kwamba walimengu hawana tena muda wa kupoteza katika kulishughulikia suala hili. Aliyataka Marekani, Uchina, Bara Hindi, mataifa ya Umoja wa Ulaya pamoja na nchi nyingi nyenginezo - zote zijumuike kwenye juhudi za kukabiliana na suala hili, haraka, na alihimiza Mataifa Wanachama kuzisaidia, kihali na mali, zile nchi maskini zilizonyimwa kabisa uwezo wa kujirekibisha kimaendeleo, kutokana na athari mbaya za hali ya hewa.