Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mobutu na Tshombe, viongozi wa DRC waliotwamisha nchi yao

Picha:UN/Maktaba
Joseph-Desiré Mobutu enzi zake.

Mobutu na Tshombe, viongozi wa DRC waliotwamisha nchi yao

Amani na Usalama

Joseph-Desiré Mobutu, alikuwa Rais wa Zaire zamani ikijulikana Congo, na sasa DR Congo kwa miaka 32. Moise Tshombe, Rais wa kwanza na pekee wa jimbo la Katanga lililojitenga. Wawili hawa walikuwa chachu kubwa katika kizazi cha kusaka uhuru barani Afrika.

Joseph-Desiré Mobutu, alikuwa Rais wa Zaire zamani ikijulikana Congo, na sasa DR Congo kwa miaka 32. Moise Tshombe, Rais wa kwanza na pekee wa jimbo la Katanga lililojitenga. Wawili hawa walikuwa chachu kubwa katika kizazi cha kusaka uhuru barani Afrika.

Wakati akiwa madarakani, Mobutu alikuwa mwerevu, lakini asiyependeka sana na ni wakati wa kipindi chake aliweza kusambaratisha taifa ambalo yawezekana kuwa la tatu kwa kuwa na utajiri zaidi Afrika.

image

Moise Tshombe enzi za uhai wake. (Picha:UN/Maktaba)

Kipindi cha uongozi cha Moise Tshombe kilikuwa kifupi lakini uongozi wake katika kujitenga kwa jimbo la Katanga lenye madini mengi, ulitumbukiza nyongo matamanio ya wananchi kuhusu mustakhbali wa Congo.

Brian Urquhart, mtumishi wa Umoja wa Mataifa ambaye ndiye mwandishi wa simulizi hizi anaeleza kuwa alipokutana na Mobutu Julai mwaka 1960, Mobutu alikuwa ni msaidizi mkuu wa kijeshi wa Waziri Mkuu Patrice Lumumba, na alikuwa amejipandisha cheo kutoka sajini kuwa luteni kanali.

Kwa kulinganisha, Mobutu alikuwa msingi wa vitendo na maarifa ya kawaida. Walinzi wa Umoja wa Mataifa au wananchi walipokamatwa na askari wa Lumumba, Mobutu alikuwa ndio kimbilio la Umoja wa Mataifa.

Alionekana kuwa mtu wa fikra sahihi ambaye hata watu waliamini kuwa analinda maslahi ya taifa lao changa.

Mapema Septemba 1960, baada ya Rais Joseph Kasavubu kumfukuza kazi Lumumba na Lumumba kudai kumfuta kazi Rais Kasavubu, uvumi ulienea mji wa Leopoldville, na Umoja wa Mataifa ukisakwa kwa msaada. Bila kutarajia, Kanali Joseph Mobutu akiwa amevalia mavazi ya kiraia alifika mbele ya umati wa watu akiomba Umoja wa Mataifa umsaidie kuondoka nchini humo kwani alikuwa amechoka.

Mkuu wa operesheni za Umoja wa Mataifa nchini humo wakati huo Rajeshwar Dayal akamsihi Mobutu asiondoke bali asalie kusaidia nchi yake. Brian Urquhart anasema ilikuwa ni hila!

Siku mbili baadaye Mobutu akiwa na sare za jeshi alifika makao makuu ya ofisi ofisi za Umoja wa Mataifa Leopoldville akidai kuchoka na makelele na anataka sehemu tulivu, hivyo akawekwa ndani ya chumba cha mtumishi mmoja wa Umoja wa Mataifa, akipatiwa pombe kali huku akisikiliza radio.

Akionekana kufuruahi muziki wa mtindo wa Cha Cha cha, ghafla radio Leopoldville ikanyamaza kucheza muziki na sauti ikatoka ikitangaza kusimamishwa kwa Rais, Waziri Mkuu na bunge na kwamba mtu huyo anayetangaza ndiye amechukua nchi.

Ni mimi, Mobutu alisikika akisema! Akiruka kwa ushindi na kuelekeza kidole kwenye radio.. ni mimi! Brian Urquhart ambaye ndiye alimpatia chumba apumzike! Alishikwana hasira akimweleza Mobutu kuwa kama ni sehemu ya kutangaza mapinduzi ya kijeshi ni mitaani na wafuasi wake na si kwenye chumba chake cha kulala.

Mobutu aliondolewa pale na yasemekana kitendo alichofanya kilipatiwa nguvu na Marekani na hakikuwa cha kikatiba. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo Dag Hammarskjold na wawakilishi wake Congo walikataa kumtambua kuwa ni rais.

image

Oktoba 04, 1973, Rais Mobutu Sese Seko akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani. (PICHA:UN/Yutaka Nagata)

Mabalozi wa Marekani na Uingereza huko Leopoldville walipinga uamuzi wa Umoja wa Mataifa wakisema Mobutu alikuwa si mkomunisti na anafaa kwa kuongoza Congo.

Mobutu alibadili jina lake na kujiita Mobutu See Seko Kuku Ngbendu ikimaanisha, “Mpiganaji anayeshinda kila vita na kuacha moto kila apitapo au jogoo asiyeacha kuku jike peke yake. Na vazi lake tambulishi la kofia ya ngozi ya chui na ndege yake Boeing 747 inayobeba ujumbe wake, bila shaka alikuwa dikteta wa aina yake. Brian anasema walikutana uso kwa uso wakati wa hafla moja, ambapo Mobutu alikumbuka urafiki wao mwanzoni kabisa mwa uhuru wa Congo, ambapo alisema kuwa Brian hakuwa mwema mara ya mwisho walipokutana.

image

Septemba 14, 1979 Mobutu alipokutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo Kurt Waldheim jijini New York, Marekani. (Picha: UN /Saw Lwin)

Mwaka 1997, Mobutu alipofariki dunia kutokana na saratani, nchi yake ilikuwa katika sintofahamu na mapinduzi yalimweka madarakani Laurent Kabila.

Moise Tshombe angalau aonekana kuwa alikuwa na unafuu kuliko Mobutu na hakuonekana kuwa msaka pesa kama Mobutu. Kampuni kubwa ya madini iitwayo Union Minière, ilimbaini Tshombe kuwa ndio chambo chao cha kujipatia mali za madini kutoka Katanga, Congo hata baada ya uhuru.

Wakati wa Uhuru, Tshombe alikuwa Rais wa jimbo la Katanga, na siku kumi baadaye, chini ya usaidizi wa Ubelgiji, Katanga ikajitangaza jimbo huru.

Kampuni za madini pamoja na serikali ya Ubelgiji zilimpatia pesa nyingi sana Tshombe, ambapo kiasi kikubwa kilielekezwa kwenye akaunti zake huko benki za Uswisi. Alikuwa na washauri kutoka Ulaya, walinzi kama wale wa kitaifa wa Ufaransa wakiwa na kofa za aina yake. Suti zake zilikuwa za kushoneshwa kutoka London na Paris na washauri walihakikisha Katanga inapata bendera yake, halikadhalika stempu, sarafu na hata wimbo wa jimbo.

image

Tarehe 21 Disemba 1961, kikao kilichoandaliwa na ONUC ambapo Waziri Mkuu wa Congo, Cyrille Adoula na Moise Tshombe ambaye alikuwa Rais wa jimbo la Katanga katika kikao kwenye makao makuu ya kituo cha anga cha Umoja wa Mataifa, huko Kitona, kusini-magharibi mwa Congo, sasa DRC. (PICHA: UN/BZ)

Baada ya Umoja wa Mataifa kufanikiwa kuondoa jeshi la Ubelgiji kutoka Katanga, wanamgambo wa Tshombe walikuwa ni maafisa wa Ubelgiji ambao walikuwa ni askari kanzu na mamluki wengineo kutoka vikosi vya parachuti vya Ufaransa huko Algeria.

Katanga ikiendelea kuwa imejitenga, maeneo mengine ya nchi hayakuwa tulivu na wengi serikalini na hata ndani ya Umoja wa Mataifa walipinga kujitenga kwa jimbo hilo, ilikuwa ni lazima kupata suluhu.

Ukosefu wa jeshi lenye nguvu, ulilazimu mashauriano na kikosi kisichotumia nguvu. Baaada ya kifo cha Lumumba, Umoja wa Mataifa uliidhinisha kikosi cha Umoja wa Mataifa kutumia nguvu au kukamata mamluki. Novemba 1961, baada ya jitihada za kijeshi na kidiplomasia kushindikana na Hammarskjold kufariki dunia kwenye ajali ya ndege akielekea kwenye mazungumzo na Tshombe, Brian ambaye ni msimulizi wa kisa hiki anasema alitumwa Katanga kujaribu kuwaleta kwenye meza ya pamoja Tshombe na serikali kuu.

Katika mlo wa kwanza wa jioni Katanga, Brian alitekwa na kupigwa na askari wa Tshombe ambaye alilazimika kutumia ushawishi wake ili aachiwe tayari kwa mazungumzo kati yao siku mbili baadaye.

image

Tarehe 26 Machi mwaka 1962, moja ya gwaride la jeshi la serikali ya Congo, kuaga makamanda wa kikosi cha Umoja wa Mataifa. Mmoja wa wageni ni Kanali Mobutu ambaye amesimama mbele ya mlingoti wa bendera. (PICHA:UN/ BZ)

Brian anasema lengo lake lilikuwa ni kuwezesha Tshombe kuafikiana na serikali kuu ya Congo na kumaliza kujitenga kwa Katanga. Anasema alimweleza kuwa akifanya hivyo, anaweza kuwa Waziri Mkuu wa Congo, jambo ambalo alikuwa miaka miwili baadaye.

Hata hivyo mwaka 1965, mwaka mmoja baada ya kuwa Waziri Mkuu, Tshombe alipinduliwa na harakati zilizoongozwa na mamluki baada ya Umoja wa Mataifa kuondoka Congo.

Tshombe alikimbilia Hispania, ambako aliweza kutumia pesa zake kutoka akaunti za Uswisi akipatiwa ulinzi na serikali.

Akiwa Hispania, mwaka 1967 alilaghaiwa na kupelekwa Algeria kwa lengo la kuwa kiongozi wa vuguvugu la vijana.

Tshombe aliishia kuishi Algeria ambapo aliishi kianasa lakini katika eneo lililokuwa limehifadhiwa kwa ajili ya wafungwa wa kisiasa. Alipofariki dunia mwaka 1969 kutokana na ugonjwa wa moyo kulikuwepo na vurugu ya aina yake ya kugombea fedha zake kwenye benki ya Uswisi.

image

13 Septemba 1961 – Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Dag Hammarskjöld (kulia, mbele) akiwakagua walinzi wa heshima kwa uwanja wa ndege huko Congo alipotua mji mkuu, iliojulikana kama Leopoldville. Katikati ni Waziri Mkuu Cyrille Adoula na kushoto, Kanali Joseph Mobutu. picha: UN Photo/BZ