Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

KM ametoa taarifa yenye kubainisha wasiwasi alionao juu ya kupwelewa kwa huduma za misaada ya kihali Zimbabwe kutokana na vikwazo vilioekewa mashirika yasio ya kiserikali na wenye madaraka mnamo Juni 2008.

Alisema maombi kadha yalitumiwa Serikali na Timu ya Maofisa Wakazi Zimbabwe na washirika wengine wanaohudumia misaada ya kiutu lakini operesheni za mashirika yasio ya kiserekali na yale ya khiyari bado zimepigwa marufuku kwa sasa hivi, hali ambayo imesababisha mashirika ya UM kuhudumia watu 280,000 badala ya umma muhitaji milioni 1.5 katika Zimbabwe. KM ameinasihi Serikali iondoshe vikwazo hivyo haraka na kuyawezesha mashirika ya kimataifa kutekeleza majukumu yao ya kuhudumia misaada ya kiutu ili kunusuru umma husika na janga la kiutu linalobashiriwa kujiri pindi hali hii itashindwa kurekibishwa haraka.

Shirika la Ulinzi Amani katika JKK (MONUC) limekamilisha mafunzo ya miezi mitatu ya kijeshi kwa batalioni mbili za Jeshi la Kongo, kitendo ambacho kiliadhimishwa rasmi Ijumatano kwenye sherehe maalumu iliofanyika katika kambi ya jeshi ya jimbo la Kivu Kusini. Mjumbe Malumu wa KM kwa JKK na Mkuu wa MONUC, Alan Doss, kwenye hotuba alioitoa kwenye taadhima hizo alisisitiza mafunzo ya kijeshi yanayotolewa na UM yamesaidia kutekeleza maazimio ya kuleta mageuzi yenye natija kwenye jeshi la taifa katika kudhibiti usalama na amani. Mafunzo hayo yalipatiwa askarijeshi 1,800 na yalijumuisha masomo kuhusu mbinu za kijeshi, namna ya kudhibiti silaha, maadili ya kitaaluma na taratibu za kuimarisha miundombinu kijumla. Mpaka sasa MONUC imefanikiwa kukamilisha mafunzo haya ya kijeshi kwa batalioni 12 za Jeshi la Kongo, na inalenga kukamilisha masomo kwa batalioni 28 mnamo mwezi Septemba mwakani.

Ashraf Qazi, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Sudan alipokutana na waandishi habari Alkhamisi mjini Khartoum alitangaza kuwa na wasiwasi kwamba mpango wa amani nchini unaonyesha “kuregarega”, hususan baada ya kundi la waasi la JEM lilipoamua kushambulia mji wa Omdurman, karibu na Khartoum na baada ya kufumka mapigano kwenye mji wa Abyei mwezi Mei, ambapo makumi elfu ya raia walhajiri makazi, kutoka eneo lenye utajiri mkubwa wa petroli. Qazi alikumbusha kihakika kwamba amani ya Sudan si ya kugawanyika, si katika eneo la kaskazini, kusini wala Darfur, kwa sababu usalama wa maeneo yote hayo unafungamana na unategemea kutekelezwa kwa kuambatana na vibwagizo vilivyoidhinishwa kwenye Mapatano ya Amani ya Jumla (CPA). Alisema ni matumaini yake ramani ya mapatano ya Abyei itatumiwa kuchochea juhudi ziada za kuleta suluhu kwenye yale masuala yaliosalia yenye utata, kwa kulingana na mfumo wa Mapatano ya CPA.