Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

KM Ban Ki-moon amekaribisha mapatano ya kusitisha kwa muda wa miezi sita uhasama kati ya Israel na eneo la Wafalastina la Ghaza. Alitumai juhudi hizi zitaimarisha usalama na kupunguza matatizo ya kiutu katika Ghaza kwa kufungua vile vituo vya ukaguzi ili kuruhusu shughuli za kibiashara kuendelezwa bila vizuizi. Kadhalika KM alinasihi mashambulio ya makombora ya kienyeji dhidi ya Israel yakomeshwe.

Shirika Mseto la UM/AU kulinda amani Darfur (UNAMID) limeripoti ya kuwa mmoja wa mfanyakazi wao alitekwa nyara mita 10 kutoka kambi ya majeshi ya kimataifa katika mji wa ElGenina, karibu na uwanja wa ndege, na kunyanganywa vitu vyake, na vya kazi, na pia kupigwa na kuumizwa mwili na wanamgambo hao. Wenziwake watatu wengine walishikwa na kutishiwa kupigwa risasi. UNAMID iliripoti kwamba baada ya mtumishi wa Usalama wa Taifa Sudan kuingilia kati washambulizi wa mfanyakazi UNAMID waliamua kumwachia huru. Wanajeshi wa mgambo hawa wanaripotiwa na UNAMID kuwa waliandamana kwenye msafara wa karibu watu 1,000 waliopanda ngamia, farasi na magari ya magurudumu manne, wakionekana wakielekea Makao Makuu ya Vikosi vya Jeshi la Sudan.

Maofisa wa UM katika Chad wamearifu hali ya usalama mashariki-kaskazini ya nchi ni shwari kwa sasa, kufuatilia mapigano ya silaha katika siku za karibuni, kati ya makundi ya upinzani na vikosi vya Serikali. Wahudumia misaada ya kiutu wa UM wamenasihiwa kuelekea sehemu nyengine za nchi kuwasaidia wahamaiji wa ndani wa Chad pamoja na wale wa kutokea Darfur, Sudan wanaoishi kwenye kambi ziliopo karibu na mji wa Goz Beida.

Ripoti ya mwezi juu ya hali ya haki za binadamu katika JKK, iliotolewa na MONUC, imenakiliwa ikishtumu makundi ya kigeni, na ya kienyeji, yenye silaha kuwa ndio yenye kusababisha kuharibika kwa usalama na haki za binadamu katika sehemu kadha za nchi. Kadhalika jeshi la serikali pamoja na polisi nawo pia wamekutikana kukiuka haki za raia, vitendo ambavyo vile vile vinajumuisha hujuma za kunajisi kimabavu wanawake na kufanya mateso dhidi ya umma.

Baraza la Haki za Binadamu (HRC) lilitarajiwa kukamilisha kikao cha 8 mjini Geneva alasiri baada ya kupitisha maazimio na maamuzi 15 yanayoambatana na kanuni za kutunza haki za binadamu ulimwenguni.

Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu, Louise Arbour amepongeza uamuzi wa Baraza la Haki za Binadamu (HRC) wa kupitisha chombo muhimu cha sheria ya kimataifa chenye lengo la kuimarisha bora hifadhi ya haki za kiuchumi, kijamii na kitamaduni.