Skip to main content

Hapa na pale

Hapa na pale

Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) limewaslisha wiki hii mjini Roma, Utaliana ripoti yenye mada isemayo "Hali ya Misitu Duniani 2007". Ripoti ilisema maeneo kadha duniani yamefanikiwa kudhibiti uharibifu wa misitu ulioendelezwa karne kwa karne. Kwa mujibu wa ripoti misitu kadha imefanikiwa kufufuliwa na kupanuliwa kwenye kanda mbalimbali za kimataifa kwa sababu ya usimamizi mzuri, na wa hadhari, ikichanganyika na sera za kisasa zilizotumiwa na mataifa husika katika kuhifadhi mazingira kwa ujumla. Ripioti ilisema mataifa 100 ziada hivi sasa yameandaa mipango ya kizalendo kuhifadhi misitu.

Jan Egeland wa Norway, aliyekuwa Mkuu wa Ofisi ya UM juu ya Huduma za Dharura (OCHA) ameteuliwa na KM Ban Ki-moon kuwa Mshauri Maalumu juu ya masuala yanayohusu sera za kuzuia na kusuluhisha migogoro duniani.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limemteua, kwa mara nyengine tena, Liya Kebede wa Ethiopia kuwa Balozi Mfadhili atakayepigania haki za kuboresha afya za mama na watoto, hususan katika kukabiliana na matatizo yanayochochewa na uzazi.