Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Juhudi za kidiplomasiya zachacha kusuluhisha mzozo wa Darfur

Juhudi za kidiplomasiya zachacha kusuluhisha mzozo wa Darfur

Tume ya Baraza la Haki za Kibinadamu iliyodhaminiwa madaraka ya kufanya uchunguzi kuhusu utekelezaji wa haki za kimsingi katika Darfur, majuzi ilichapicha ripoti yenye kuishinikiza Serekali ya Sudan kuharakisha uamuzi wa kuisaidia Umoja wa Mataifa (UM) pamoja na Umoja wa Nchi Huru za Afrika (AU)kupeleka vikosi vya mseto vitakavyotumiwa kulinda amani katika jimbo la Sudan magharibi la Darfur.

Wajumbe wa tume hiyo walishindwa kuzuru Darfur baada ya Serekali ya Sudan ilipokataa kumpatia mmoja wao viza ya kuingilia nchini. Ujumbe wa Tume ulitembelea mataifa jirani, badala yake, na kuendeleza uchunguzi miongoni mwa raia wa Darfur wanaoishi kwenye kambi za wahamiaji.

•Waziri wa Sheria wa Sudan, Mohamed Ali ElMardi alikutana na waandishi habari mjini Geneva wiki hii na alisema Serikali yake imenuia, kithabiti, kupokea vikosi vya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (AU) pekee kulinda amani katika Darfur; na alisisitiza kwamba ni wajibu wa UM kuvipatia vikosi vya AU uwezo na vifaa vinavyohitajika kuimarisha usalama na amani katika Darfur. Kadhalika, kwenye kikao cha Baraza la Haki za Binadamu kilichofanyika wiki hii Geneva kuzingatia ripoti ya Tume juu ya Darfur, Waziri ElMardi aliwaambia wajumbe waliohudhuria mkutano ya kuwa Serekali ya Sudan haitambui hitimisho ya ripoti hiyo, na alisisitiza kwamba ripoti haina “hadhi ya kisheria, na wala si halali.”

•KM Ban Ki-moon alipokutana na waandishi habari kwenye Makao Makuu ya UM alisema hakufurahika na jawabu ya barua aliyotumiwa na Raisi Omar Hassan AlBashir wa Sudan, juu ya pendekezo la kupeleka vikosi vya mseto vya UM na AU katika Darfur, na alitilia mkazo jawabu hiyo ilikuwa “hairidhishi”. Alisema jumuiya ya kimataifa inaanza kukata tamaa na uwezekano wa kukomesha vurugu la Darfur kwa utaratibu uliokubaliwa kabla.

•Louise Arbour, Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu aliwazindua wajumbe waliohudhuria mijadala ya Baraza la Haki za Binadamu mjini Geneva kwamba matatizo ya ukiukaji wa haki za kimsingi kwa umma ni masuala yanayohusu kila taifa katika pembe zote za ulimwengu. Alisema nchi wanachama zitafaidika pakubwa pindi zitashirikiana na kujihusisha kikamilifu na mfumo wa kimataifa wa kuimarisha haki za kibinadamu kwa umma.