Palestina na Israeli wakae meza moja kumaliza tofauti zao : Guterres
Baraza kuu la Umoja wa Mataifa limekutana leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya kuonyesha mshikamano na wapalestina, ili kujadili mustakabali wa eneo hilo ambalo limekuwa katika migogoro kwa miongo zaidi ya mitano.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, kupitia naibu wake, Amina J. Mohammed, amerejelea wito wake kwa waisreli na wapalestina kukaa meza moja na kutafuta suhulu ya mgogoro uliodumu kwa kipindi kiferu sasa.
Bi. Amina amesema suluhu ya mataifa mawili kati ya Israeli na Palestina ni miongoni ya masuala ambayo Umoja wa mataifa haujapatia ufumbuzi, hivyo maendeleo ya wapalestina yanaathirika zaidi kuliko kwa Israeli.
“Miaka 70 iliyopita tangu kupitishwa kwa azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa namba 181 ambalo ni suluhu ya mataifa mawili, bado hatujafikia hatua ya kuwa na taifa huru la wapalestina sambamba na taifa la Israel. Ila bado naamini kwamba utekelezaji wa azimio hilo la uwepo wa mataifa mawili kati ya wapalestina na waisraeli unawezekana endapo pande zote zitakaa meza moja na kutafuta suluhu itakayosababisha amani na utulivu katika ukanda wa Mashariki ya Kati.