Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya waliokufa Syria kutokana na mapigano yakaribia 200,000

Familia wa waSyria wakijiandikisha kama wakimbizi, Halba kaskazini mwa Lebanon.© UNHCR/F.Juez

Idadi ya waliokufa Syria kutokana na mapigano yakaribia 200,000

Zaidi ya watu 191,000 wameuawa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria, kulingana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu ambapo asilimia 85 yaelezwa ni wanaume. Taarifa zaidi na Amina Hassan.

(Taarifa ya Amina)

Idadi hiyo ya vifo inatokana na ripoti kutoka vyanzo mbali mbali ikiwemo serikali na ni kuanzia mwezi Machi mwaka 2011 hadi Aprili mwaka huu wa 2014.

Hata hivyo Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay anasema idadi hiyo ya vifo pengine ni ndogo ya idadi halisi ya watu waliouawa katika kipindi hicho cha miaka mitatu ya vita Syria.

Amesema kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa kumaliza mgogoro wa Syria kumeendelea kuwapa nguvu na ujasiri wale wanaohusika katika mzozo huo.

Rupert Colville ni msemaji wa Ofisi hiyo ya Haki za Binadamu mjini Geneva.

(Sauti ya Rupert)

"Kamishna Mkuu amesikitishwa sana ya kwamba kwa kuzingatia kipindi hiki cha ukosefu wa utulivu maeneo mbali mbali, mzozo nchini Syria na madhara yake makubwa kwa mamilioni ya raia umesahaulika duniani.  Wauaji, waharibifu na watesaji wamepatiwa uwezo na kutiwa moyo na kudorora kwa hatua za kimataifa. "Kamishna Mkuu alisema. "Kuna madai makubwa ya kwamba uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu umetendeka mara kwa mara na kuna ukwepaji wa sheria, lakini Baraza la Usalama limeshindwa kuwasilisha mzozo wa Syria kwenye Mahakama ya Kimataifa  ya uhalifu, ambapo ndipo inapohitajika. Ni muhimu Serikali zichukue hatua thabiti kusitisha mapigano na kuzuia uhalifu. Na zaidi ya yote ziache kuchochea uhalifu huo mkubwa unaofanyika kwa kusambaza silaha na vifaa vingine vya kijeshi. "

Elfu Tisa kati ya waliouawa ni watoto ambapo zaidi 2,000 wana umri wa chini ya miaka kumi.

Idadi kubwa ya mauaji hayo ni kutoka viungani mwa mji mkuu Damascus watu 39,000 na Aleppo 31,000. Huko Homs 28,000, Idlib 20,000, Daraa 18,000, na Hama 14,500.