Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR na washirika wachukua hatua ya kuwasaidia wakimbizi wa Syria

UNHCR na washirika wachukua hatua ya kuwasaidia wakimbizi wa Syria

Shirika la kuhudumia wakimbizi  la Umoja wa Mataifa  UNHCR linachukua hatua za kuwalinda maelfu ya wakimbizi wa Syria walio nchini Lebanon wakiwemo wakimbizi 120,000 wanaoishi kwenye mahema wakati huu wa msimu wa baridi.

Kupitia usaidizi kutoka kwa jeshi la Lebanon, UNHCR na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali juma hili walifanikiwa kusambaza misaada zaidi kwa maelfu ya wakimbizi wanaoishi kwenye mahema katika bonde la Bekaa mashariki mwa Lebanon ambalo ni eneo lililoathiriwa na tufani kwa jina Alexa.

Makundi ya kutoa huduma za dharura yaliendelea na shughuli hata baaada ya barabara nyingi kuwa katika  hali ya kutopitika. Karibu wakimbizi 125,000 wanoishi kwenye eneo la Bekaa walipokea bidhaa za kutumia wakati wa msimu wa Baridi huku wengine zaidi wakitarajiwa kupokea misaada.

Mashirika ya kibinadamu yanayohudumu kote nchini Lebanon yamesambaza mablanketi 255,000 kwa kipindi cha majuma sita yaliyopita huku kadi za  ATM 45,000 zikiwa na dola 150 zikisambazwa kwa familia zilizo na mahitaji zaidi kuwawezesha kunua majiko na mafuta.