Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampeni yazinduliwa Sudani kukabiliana na masuala ya uhamiaji

Kampeni yazinduliwa Sudani kukabiliana na masuala ya uhamiaji

Shirika la kimataifa linalohusika na masuala ya uhamiaji IOM limezindua kampeni ya utoaji taarifa nchini Sudan kuhusu athari zitokanazo na uhamiaji holela, kama sehemu ya juhudi za kupambana na matatizo ya uhamiaji Afrika ya Mashariki na pembe ya Afrika.

Kampeni hiyo ambayo inayalenga majimbo saba mashariki mwa Sudan, itatekelezwa kama sehemu ya mpango wa IGAD kushughulikia kasoro zilizopo kwenye mfumo wa uhamiaji wa nchi wanachama .

Itakuwa na lengo la kuwafahamisha wahamiaji haramu na halali hatari itakayowakabili katika safari zao za kwenda Ulaya na Mashariki ya kati. Sudani ndio kiungo cha safari za kutoka Afrika ya Mashariki kuelekea Mediteranian. Ni moja ya njia tatu kuu zinazotumiwa na wahamiaji wa Ethiopia, Eritrea na Somalia kuelekea Ulaya wakipitia Libya na Misri. Wengi wao wanakimbia umasikini, vita na ukame unaozikabili nchi zao.