Chondechonde Hong Kong watendeeni haki wanaharakati wa demokrasia:UM
Jopo la watalam wa haki za kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wameiasa mamlaka ya Hong Kong kuheshimu ahadi zake katika kutekeleza haki za binadamu kwa wanaharakati wa kidemokrasia watatu watakaokata rufaa kupinga hukumu zao tarehe 7 Novemba.
Wanaharakati hao Joshua Wong, Nathan Law na Alex Chow walifungwa mwezi Agosti ambapo mmoja kati yao alihukumiwa kwa miezi sita na mwingine miezi mne kutokana na nyadhifa zao za kiungozi, kwa sababu ya maandamano ya mwaka 2015, ambapo waliachiwa huru kwa dhamana wakati wakisubiri rufaa .
Katika taarifa ya pamoja wataalam hao wa haki za binadamu wamesema ni lazima mahakama ya Hong Kong ifuate sheria ya kimataifa katika kuwatendea haki wahukumiwa hao na pia wametoa wito kwa mamlaka ya Hong Kong kuheshimu uhuru wa mahakama na utawala wa sheria
Aidha wataalamu hao wameitaka mamlaka ya Hong Kong kusimamia haki katika kulinda uhuru wa kujieleza na wa mikutano ya amani chini ya azimio la Kimataifa la Haki za kiraia na kisiasa, ambalo Hong Kong ni mwanachama .