Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yaadhimisha siku ya wanawake kwa kupigia chepuo usawa wa kidijitali

Sima Bahous mkurugenzi mtendaji wa shirika la umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake UN Women akihutubia washiriki kwenye Baraza Kuu la Un wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake  2023
UN Photo/Manuel Elías
Sima Bahous mkurugenzi mtendaji wa shirika la umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake UN Women akihutubia washiriki kwenye Baraza Kuu la Un wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake 2023

UN yaadhimisha siku ya wanawake kwa kupigia chepuo usawa wa kidijitali

Wanawake

Siku ya kimataifa ya wanawake iliyobeba maudhui “Dijitali kwa wote, ugunduzi na teknolojia kwa ajili ya usawa wa kijinsia imeadhimishwa leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kwa msisitizo wa haja ya ujumuishwaji wa wanawake katika elimu na mabadiliko ya teknolojia na masuala ya kidijitali.

Rais wa kikao cha 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa amewahutubia washiriki katika hafla hiyo mjini New York Marekani akisema "Nimefurahia kusherehekea siku ya kimataifa ya wanawake na kuuunga mkono wito wa uvumbuzi unaojumuisha jinsia, elimu ya kidijitali na teknolojia. Maendeleo haya yanahitaji umakini wetu kamili ikiwa tunatumai kufikia ahadi ya malengo endelevu ya maendeleo endelevu. "

Csaba Kőrösi pia amesema, "Kufikia mwaka 2050, asilimia 75 ya ajira zitahusiana na sayansi, teknolojia, uhandisi na hesabu, kama tunavyoita kwa njia fupi STEM. Leo hii bado wanawake ni theluthi moja tu ya nguvu kazi katika makampuni 20 makubwa ya teknolojia ya Ulimwengu na asilimia 57 tu ya wanawake hutumia mtandao. "

Rais huyo wa Baraza Kuu ameendelea kusema kuwa, "Ukweli huu unadhihirisha changamoto zilizo mbele yetu. Pia unazungumzia fursa kubwa zinazotolewa na uvumbuzi na teknolojia za kubadilisha haraka simulizi kwa wanawake na wasichana ifikapo 2030. "

Courtenay Rattray akiwasilisha ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake 2023
UN Photo/Manuel Elías
Courtenay Rattray akiwasilisha ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake 2023

Hatua zahitajika kuwa salama mtandaoni

Ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres uliosomwa katika hafla hiyo kwa niaba yake na Earle Courtenay Rattray, umegusia ukatili na mashambulizi yanayoendelea mtandaoni ukisistiza kwamba  ukatili dhidi ya watu mtandaoni “shambulio la moja kwa moja kwa demokrasia na unawadhibiti wanawake, kuwazuia na kuwandama kuanzia ofisini, na kuwa kigingi cha matarajio ya wasichana kujiongeza kama viongozi."

Ujumbe wake umebainisha kwamba "Tunahitaji hatua kuweka mazingira salama ya kidijitali na kushikilia wanyanyasaji, wafanya ukatili na majukwaa ya kidijitali ambayo yanawawezesha wanyanyasaji hao.”

Pia ameongeza kuwa “Ndio sababu nimetoa wito kwa serikali, wasimamizi wa mitandao, makampuni ya teknolojia na vyombo vya habari kuzuia chuki, kuanzisha walinzi, na kutekeleza wito huo. Na ndio sababu tunafanya kazi kuendeleza kanuni za mwenendo wa uadilifu wa habari kwenye majukwaa ya kidijitali. "

Mkokotoa hesabu mjini Kigali Rwanda akiunda apu ili kuchagiza masuala ya kuweka akiba na uhuru wa masuala ya fedha
© UNICEF/Mary Gelman
Mkokotoa hesabu mjini Kigali Rwanda akiunda apu ili kuchagiza masuala ya kuweka akiba na uhuru wa masuala ya fedha

Unyanyasaji na ubaguzi dhidi ya wanawake lazima ukome

Mathu Joyini, mwenyekiti wa kikao cha 67 cha kamisheni ya hali ya wanawake duniani pia amezungumza na washiriki akisema, "Kwa mara nyingine tena hebu nitumie siku hii kuelezea mshikamano wangu na wanawake wote walio kwenye maeneo yenye migogoro na maeneo yaliyoathirika na janga. Fikra zetu zipo Pamoja nanyi katika siku hii, na tunaendelea kuwatakia nguvu na ujasiri. "

Kwa upande wake mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake UN Women Sima Sami Bahous amegusia maswala yanayohusiana na unyanyasaji, akisema, "Wanaharakati wa masuala ya wanawake wako kila mahali wamesimama imara. Kwa wito wa kukomesha unyanyasaji, vurugu, ubaguzi katika elimu, mahali pa kazi, katika sheria, na katika nyanja zote za maisha yao. Leo, siku ya kimataifa ya wanawake, hebu tuthibitishe azimio letu la kuheshimu kazi ya ujasiri na isiyo ya kuchoka ya wanawake hawa wote. "

Kikao cha 67 cha Tume ya Hali ya Wanawake kinafunguliwa katika ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York.
UN Photo/Manuel Elías
Kikao cha 67 cha Tume ya Hali ya Wanawake kinafunguliwa katika ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York.

Naye Amina J. Mohammed, naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amesema, "Mitandao na huduma za mawasiliano ya ICT kuwezesha ukatili wa misingi ya kijinsia, imewaweka wanawake na wasichana katika hatari katika majukwaa ya kidijitali. Bila hatua madhubuti mgawanyiko wa kijinsia wa kidijitali utakuwa sura mpya ya kupanua wigo wa pengo la usawa wa kijamii na kiuchumi. "

Hafla hiyo ya ngazi ya juu imewaleta pamoja wataalam wa teknolojia, wavumbuzi, wajasiriamali, na wanaharakati wa usawa wa kijinsia kutoa fursa ya kupigia chepuo jukumu la wadau wote katika kuboresha fursa za ufikiaji wa zana za kidijitali.