Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wasichana wanachohitaji ili kukumbatia ICT ni fursa na usalama mtandaoni: ITU 

Wasichana wakiwa shuleni Yaoundé mji mkuu wa Cameroon wakisoma kutumia teknolojia ya kidijitali.
© UNICEF/Frank Dejongh
Wasichana wakiwa shuleni Yaoundé mji mkuu wa Cameroon wakisoma kutumia teknolojia ya kidijitali.

Wasichana wanachohitaji ili kukumbatia ICT ni fursa na usalama mtandaoni: ITU 

Utamaduni na Elimu

Katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya wasichana katika tasnia ya Habari na teknolojia ya mawasiliano ICT muungano wa kimataifa wa mawasiliano ITU umesema fursa na usalama mtandaoni ambayo ndio maudhui ya siku ya mwaka huu ni ufunguo wa kukiingiza kizazi kijacho cha wasichana katika Habari na teknolojia ya mawasiliano.

Kwa mujibu wa ITU maudhui hayo yanaonyesha nia ya pamoja ya dunia katika kuwawezesha vijana na wasichana kufaidika kwa usalama kutokana na maisha ya kidijitali. 

ITU inatambua haja ya kuhakikisha wasichana na wanawake wanafurahia fursa sawa za kujifunza kidijitali, hasa katika nchi zinazoendelea. 

Kulingana na takwimu za hivi karibuni za ITU, duniani kote, asilimia 57 ya wanawake ndio wanatumia Intaneti  duniani ikilinganishwa na asilimia 62 ya wanaume.  

Na duniani kote ni asilimia 30 tu ya wataalamu wa sayansi ya teknolojia na tasnia ya teknolojia ni wanawake.  

Ikiwa wanawake hawawezi kufikia mtandao na hawajihisi salama mtandaoni, hawawezi kukuza ujuzi muhimu wa kidijitali na kujihusisha katika nafasi za kidijitali, jambo ambalo linapunguza fursa zao za kuingia katika tasnia za teknolojia, uhandisi na hisabati au STEM. 

Doreen Bogdan-Martin, ni mkurugenzi wa kitengo cha maendeleo ya mawasiliano wa ITU. amesema "Ulimwenguni kote, wasichana na wanawake wanataka kujiunga na mapinduzi ya kidijitali. Tunapoondoa vikwazo vya fursa za ufikiaji na usalama, wanawake na wasichana wanaweza kutoa mchango mkubwa na kuwezeshwa na ICT. Kwa kifupi teknolojia inahitaji wasichana, na wasichana wanaihitaji teknolojia," 

Hivyo amesesisitiza kuwa,“Kwenye siku hii ya wasichana katika ICT hebu tufanye kazi pamoja kuhakikisha kwamba kila msichana na kila mwanamke kila mahali anapata fursa ya kutumia teknolojia ya kidigitali kustawi, kutimiza ndoto zake na kuwa katika ubora wake” 

Naye Katibu Mkuu wa ITU Houlin Zhao katika ujumbe wake wa siku hii amesema “Siku ya wasichana katika ICT ni wito wa kuchukua hatua kuhamasisha kizazi kijacho cha vijana wa kike na wasichana kuingia katika taaluma ya STEM, natoa wito kwa viongozi wote wa serikali, wafanyabiashara, vyuo vikuu na wengine kufanya kila wawezalo kusaidia vijana wa kike na wasichana na kuwapa nafasi ya kutimiza ndoto zao." 

Siku ya kimataifa ya wasichana katika ICT huadhimishwa kila mwaka katika Alhamisi ya mwisho ya mwezi Aprili na hadi kufikia leo zaidi ya wasichana na wanawake 600,000 wameshirikia hafla zaidi ya 12,000 za wasichana katika ICT katika nchi 195 kote duniani.