Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO: Mafanikio ya elimu yanatatizwa na ukosefu wa uwekezaji katika afya na lishe

Msichana akinywa maji katika  bustani wa shule yake huko Goré, kusini mwa Chad.
© UNICEF/Frank Dejongh
Msichana akinywa maji katika bustani wa shule yake huko Goré, kusini mwa Chad.

UNESCO: Mafanikio ya elimu yanatatizwa na ukosefu wa uwekezaji katika afya na lishe

Utamaduni na Elimu

Wakati kuwekeza katika afya na lishe shuleni kuna athari chanya kwa ufaulu wa watoto kitaaluma, shule 1 kati ya 3 duniani bado haina maji ya kunywa na vifaa vya msingi vya usafi wa mazingira, kulingana na ripoti mpya iliyozinduliwa leo 8 Februari na mashirika ya Umoja wa Mataifa la elimu , sayansi na utamaduni UNESCO, la kuhudumia watoto UNICEF, na la mpango wa chakula duniani WFP.

Audrey Azoulay, mkurugenzi mkuu wa UNESCO amesema “Wanafunzi hujifunza vyema katika shule salama na zenye afya. Bado taasisi nyingi za elimu hazina njia za kuhakikisha afya njema na ustawi, ikiwa ni pamoja na maji muhimu ya kunywa na vifaa vya usafi kama vyoo. UNESCO na washirika wake wanatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kusaidia nchi katika uwekezaji wao kwenye afya, lishe na ulinzi wa kijamii shuleni kwa sababu watoto wanastahili mazingira ambayo wanawawezesha kufikia uwezo wao kamili,"

Mlo shuleni ni muhimu hususan kwa watoto maskinia
WFP/Sierra Leone
Mlo shuleni ni muhimu hususan kwa watoto maskinia

Kuhusu ripoti

Ripoti hiyo, ‘Tayari kujifunza na kustawi: Afya na lishe shuleni duniani kote’ inaonyesha kuwa hakikisho la afya na lishe shuleni linawapa motisha watoto kuja shuleni, na kubaki huko.

Milo ya shule pekee huongeza viwango vya uandikishaji wanafunzi kwa asilimia 9 na mahudhurio kwa asilimia 8.

Ripoti inasema “kupunguza minyoo na kuongeza virutubisho kunaweza kusababisha wanafunzi kuhudhuria shule kwa miaka 2.5 ya ziada katika maeneo ambayo upungufu wa damu na maambukizi ya minyoo vimeenea. Ripoti hiyo pia inazungumzia masuala mengine kama vile kukuza huduma ya macho, afya ya akili na ustawi wa watoto na kuzuia ukatili shuleni.”

Ripoti inasisitiza kwamba “Hatua hizi zote zinawakilisha faida kubwa katika uwekezaji kwa nchi, pamoja na kuboresha maisha ya kila siku na hali za masomo za watoto. Kwa mfano, programu zamlo shuleni huleta faida ya dola 9 kwa kila dola1 iliyowekezwa, na programu za shule zinazoshughulikia afya ya akili zinaweza kutoa faida ya uwekezaji ya dola 21.5 kwa kila dola1 iliyowekezwa.”

Uwekezaji haba na usio sawa

Ripoti imesisitiza kuwa ikiwa nchi 9 kati ya 10 duniani kote zitawekeza katika programu za afya na lishe shuleni, uwekezaji huu hauna usawa kutoka eneo moja hadi jingine na mara nyingi hautoshi ikilinganishwa na mahitaji.

Hivyo imesenma “Kujitolea zaidi kutoka kwa serikali za kitaifa na msaada kutoka kwa jumuiya ya kimataifa ni muhimu. Ulimwenguni, kote ni dola za Marekani bilioni 2 pekee zinazowekezwa kila mwaka katika kushughulikia mahitaji ya kiafya ya watoto na vijana walio katika umri wa kwenda shule, ambapo baadhi ya dola bilioni 210 hutumika kuelimisha kundi hili katika nchi za kipato cha chini-kati na cha chini.”

Hivi sasa, kwa mujibu wa ripoti karibu shule 1 kati ya 3 (31%) hazina maji safi ya kunywa na vifaa vya msingi vya vyoo.

“Hii ina maana kwamba wastani wa watoto milioni 584 wana upatikanaji mdogo au hawana kabisa huduma za msingi za maji ya kunywa shuleni, watoto hawa 2 kati ya 5 wanaishi Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Na wakati karibu nchi zote duniani zinatoa chakula shuleni, inakadiriwa kuwa watoto milioni 73 walio katika mazingira magumu zaidi bado hawanufaiki na programu hizi za mlo shuleni.”

Watoto wakijifunza kuhusu matunda na mboga za majani katika kituo cha mafunzo ya watoto wadogo nchini Rwanda. (maktaba)
UNICEF/Veronica Houser
Watoto wakijifunza kuhusu matunda na mboga za majani katika kituo cha mafunzo ya watoto wadogo nchini Rwanda. (maktaba)

Suluhu za bei nafuu za kukidhi mahitaji

UNESCO, UNICEF na WFP zinatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, nchi na washirika kuchukua hatua ili kulinda na kukuza afya ya kimwili na kiakili, lishe, ustawi na maendeleo ya wanafunzi wote.

Wadau wote wanahimizwa kuzingatia hatua muhimu zinazofaa kwa mazingira na mahitaji ya ndani, zikijumuisha, utoaji wa chakula shuleni, chanjo, kukomesha tatizo la minyoo, msaada wa kisaikolojia, elimu ya afya inayozingatia ustadi ambayo inawawezesha wanafunzi kuishi maisha yenye afya na mazingira salama na jumuishi ya kujifunzia ambayo yanakuza afya na ustawi.