Skip to main content

Mashirika ya UN yapambana na utapiamlo shuleni Guatemala 

Nchini Guaemala WFP ikisambaza chakula kwa jamii za asili ambao wameathirika na ukosefu wa uhakika wa chakula kufuatia athari za kijamii za COVID-19
WFP/Carlos Alonzo
Nchini Guaemala WFP ikisambaza chakula kwa jamii za asili ambao wameathirika na ukosefu wa uhakika wa chakula kufuatia athari za kijamii za COVID-19

Mashirika ya UN yapambana na utapiamlo shuleni Guatemala 

Msaada wa Kibinadamu

Guatemala ni taifa linaloshika nafasi ya 4 kwa kuwa na viwango vya juu vya utapiamlo duniani, lakini sasa kwa msaada wa mashirika ya Umoja wa Mataifa lime la mpango wa chakula duniani WFP, la chakula na kilimo FAO na mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo IFAD changamoto hiyo inadhibitiwa kwa kuhakikisha mlo shuleni.

Mji wa San Marcos Guatemala ni moja ya miji iliyoathirika sana na utapiamlo nchini Guatemala.  

Kwa mujibu wa takwimu za serikali na shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO zaidi ya asilimia 50 ya watoto wa chini ya umri wa miaka mitano wamedumaa kwa sababu ya kukosa lishe bora. 

Lakini sasa asante kwa wakulima kama ambao wanasambaza chakula chenye lishe bora katika shule mbalimbali mjini San Marco ili kupambana na utapiamlo mashuleni kupitia mradi wa usambazaji chakula mashuleni ulioanzishwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa WFP,  FAO na IFAD

Watoto wengi katika mji huu hawana lishe ya kutosha nyumbani na wengi huenda shule na njaa. Mradi wa mashirika haya unawawezesha wakulima kuzalisha na kusambaza matunda na mbogamboga kwa ajili ya mlo wenye lishe mashuleni.  

Yulissa Molares ni Rais wa jumuiya ya shule na wazazi San Marcos anasema,“Miaka saba iliyopita tulishuhudia kiwango cha juu zaidi cha utapiamlo katika jamii hii, kwa sababu familia zina hulka ya kuwa na watoto wengi na hazina chakula cha kutosha kuwagawia wote” 

Miaka mitano iliyopita serikali ya Guatemala ilichukua hatua kukabili changamoto hiyo kwa kupitisha sheria ya mlo shuleni ambayo imemuwezesha kila mtoto kupata chakula chenye lishe bora shuleni kila siku, lakini bila mkakati maalum ilikuwa mtihani.

Ndio maana mwaka 2019 IFAD kwa kushirikiana na WFP na FAO wakaanzisha mkakati uliounganisha shule, wakulima na familia, na kuwapa wakulima mkataba wa kuzalisha na kusambaza mbogamboga na matunda mashuleni. 

Wazazi walifunzwa jinsi ya kutayarisha lishe bora na waalimu jukumu la kusambaza vyakula hivyo. Yulissa anaongeza,“Tulipoanza kutoa mlo shuleni, tulishuhudia Watoto walivyohamasika kuja shuleni” 

Mradi huo umekuwa neema hata wakati janga la COVID-19 shule zilipofungwa, kwani shule ziliendelea kusambaza vifurushi vya chakula kwa familia ili kuhakikisha watoto wanapata lishe inayohitajika hata wakiwa makwao.

Mradi umeendelea kuwa wa mafanikio na sasa zaidi ya familia 1,600 za wakiulima zimejiunga katika kusambaza chakula mashuleni na kupunguza kiwango cha utapiamlo nchini Guatemala.