Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Esperance Tabisha: Kutoka kuwa mkimbizi Kakuma hadi mbunifu wa mitindo Canada

Esperance Tabisha ajulikanaye pia kama Esperanza akiwa nje ya makazi yao mapya huko Ontario Canada na ni kutokana na programu ya mkimbizi kuhamia nchi ya tatu chini ya mkataba wa kimataifa wa wakimbizi wa mwaka 2018.
UN News Video
Esperance Tabisha ajulikanaye pia kama Esperanza akiwa nje ya makazi yao mapya huko Ontario Canada na ni kutokana na programu ya mkimbizi kuhamia nchi ya tatu chini ya mkataba wa kimataifa wa wakimbizi wa mwaka 2018.

Esperance Tabisha: Kutoka kuwa mkimbizi Kakuma hadi mbunifu wa mitindo Canada

Wahamiaji na Wakimbizi

Esperance Tabisha, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambaye sasa ni mnufaika wa mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi, GCR uliopitishwa mwaka 2018 wenye vipengele kadhaa ikiwemo kuhamishia wakimbizi nchi ya tatu. Alikimbia vita DRC na kuingia kambi ya Kakuma nchini Kenya mwaka 2010 na mwaka 2019 akahamia Canada kupitia msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Esperance alihamia Ontario nchini Canada akiwa na familia yake ya mume na Watoto na anasema, “Maisha yalikuwa mazuri nchini Canada hadi COVID-19 ilipoingia, tulikaa tu nyumbani na hatukujua la kufanya.”

COVID-19 ikafichua kipaji kilicho ndani yake

Kukaa nyumbani bila kufanya lolote lakini mahitaji yanatakiwa kwa ajili ya familia kulimfanya Esperance akumbushe stadi za Maisha alizojifunza akiwa nyumbani Goma jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC.

Na stadi hiyo si nyingine bali ya ushoni wa nguo ambapo anasema, “:nilitumia ujuzi wangu wa kushona nguo, na kushona barakoa ambazo nilizigawa bure kwa watu mbalimbali kama njia ya kujikinga na COVID-19.”

Ama hakika utoavyo ndivyo upatavyo, na hiyo ilidhihirikwa kwa Esperance kwani baada ya COVID-19 aliamua kuanza kushona nguo kwa wateja mbalimbali na wateja wa awali ni wale ambao aliwapatia bure barakoa wakati wa COVID-19.

Esperanza akiwa katika banda lake katika Kambi ya wakimbizi ya Kakuma, Kaskazini-Magharibi mwa Kenya
Picha/Esperanza Tabisha
Esperanza akiwa katika banda lake katika Kambi ya wakimbizi ya Kakuma, Kaskazini-Magharibi mwa Kenya

Mitandao ya kijamii imeniinua sana

Wakati anafahamisha watu kuhusu barakao anazogawa, alitumia mitandao ya kijamii kama vile Instagram na ni kupitia mtandao huo ni mingine ndiko anachapisha aina mbalimbali za mitindo anayobuni kwa ajili ya wateja wake watarajiwa na wa sasa.

“Mitandao ya kijamii imenisaidia sana kujipanua kibiashara. Nashonea nguo watu wa makabila na rangi mbalimbali na pia nasafirisha nguo kwa wateja kwenda Amerika hadi Australia,” amesema Esperance akiwa nje ya makazi yao mapya nchini Canada.

Ndani ya makazi yake, katika chumba chake cha kubuni na kushonea nguo, Esperance anaonekana akishona moja ya kitenge cha mteja wake huku nguo zingine zilizokamilika zikiwa zimening’inizwa tayari kupeleka wateja.

Mbunifu huyu wa mitindo anasema, “kazi ya kubuni mitindo na kushonga nguo imenisaidia sana kwa sababu naweza kulipa gharama za mahitaji ya nyumbani kama vile umeme na kadhalika. Na ninaipenda zaidi kwa sababu ninaifanyia hapa nyumbani nikiwa naendelea kuitunza familia yangu.”

Esperance au ukipenda Esperenza akiwa kwenye eneo lake la ushoni huko Ontario nchini Canada
UN News
Esperance au ukipenda Esperenza akiwa kwenye eneo lake la ushoni huko Ontario nchini Canada

Asante sana UNHCR kwa kunikutanisha na watu mashuhuri

Ama hakika wahenga walinena, “heshima ya kiungwana, hujua atendewayo” na ndivyo kwa Esperance hajasahau waliomvusha daraja na akiwa na tabasamu anasema, “naishukuru sana UNHCR kwa kunikutanisha na watu ambao hata sikuwahi kutarajia kukutana nao katika maisha yangu.”

Anataja watu kama Ann McCreath ambaye ni mbunifu maarufu wa mitindo nchini Kenya, “bila kusahau wana mitindo mashuhuru kama Ajuma Anasenyana na pia wakimbizi wengine kambini ambao walitusaidia ili kujiendeleza kwenye mitandao ya kijamii kupitia picha, mfano mpiga picha mashuhuri kambini Kakuma, Kenya Abdul Patience.”

Esperance anasema anashukuru sana kwa fursa walimpatia na pia “hata hapa Canada Niko leo naendelea kuona kazi nzuri wanafanya UNCHR kupitia kazi yake ya ubunifu wa mitindo.

Wito kwa wakimbizi Kakuma 

Ametoa wito kwa wakimbizi walioko Kakuma waendelee kuonesha vipaji vyao kwani vinahitajika duniani, na kwa wale waliokwenda Canada na vipaji vyao waendelee kuviendeleza na wasichoke. “Tujitahidi sisi kama wafanyabiashara na watu wenye vipaji tofauti, waimbaji na wachezaji pale kambini. Tunashukuru UNHCR ilikuwa inainua vipaji vyetu na ilihakikisha dunia nje imetujua.”

a ndoto ya Esperance ni kufahamika zaidi kimataifa ili aweze kuwavisha watu maarufu wakiwemo wanamuziki, waigizaji wa filamu halikadhalika wanasiasa!

Kuhusu Mkataba wa Kimataifa wa wakimbizi

Mkataba wa kimataifa wa wakimbizi duniani, GCR uliopitishwa mwaka 2018. ulifuatia Azimio la mwaka 2016 la New  York, kuhusu wakimbizi na wahamiaji, kwa kuzingatia kuwa ilitambulika suala la wakimbizi haliwezi kupatiwa suluhu ya kudumu na endelevu bila ushirikiano wa kimataifa. 

Mkataba wa kimataifa kuhusu wakimbizi una vipengele vikuu vinne vya usaidizi kwa wakimbizi ikiwemo mosi, kusaidia kupunguza shinikizo kwa nchi zinazohifadhi wakimbizi, pili, kuwezesha wakimbizi kujitegemea, tatu; kuhamishia wakimbizi nchi ya tatu na nne ni kuboresha mazingira ili wakimbizi waweze kurejea nyumbani kwa hiari.