Hatimaye Rahaf apata hifadhi Canada

11 Januari 2019

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limekaribisha hatua ya Canada kumpatia hifadhi na hadhi  ya ukimbizi msichana Raham Mohammed al-Qunun ambaye amekimbia ukatili kutoka kwa familia yake nchini Saudi Arabia.

Rahaf alitoroka familia yake wakati wakiwa mapumzikoni nchini Kuwait na alikimbilia Thailand.

Taarifa ya UNHCR iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi imesema hatua za haraka zilizochukuliwa wiki iliyopita na Thailand za kumpatia hifadhi ya muda ya ukimbizi na kufanikisha azma yake ya kupatiwa ukimbizi na shirika hilo, sambamba na Canada kuchukua hatua za dharura na kumpatia hadhi hiyo ya ukimbizi zimekuwa ndio msingi wa suluhisho la suala la Rahaf.

Akinukuliwa kwenye taarifa hiyo, Kamishna Mkuu wa UNHCR Filippo Grandi amesema “shida aliyokuwa nayo Rahaf kwa siku chache zilizopita imetikisa dunia nzima na kwamba hadhi ya ukimbizi hivi sasa inakumbwa na tishio na haiwezi kuwa na hakikisho. Hata hivyo katika tukio hili sheria ya kimataifa ya ukimbizi na maadili ya kibinadamu vimeshinda.,”

UNHCR inasema katika zama za sasa ambapo dunia inashuhudia katika baadhi ya nchi kushamiri kwa fikra hasi za kisiasa na mitazamo mibovu ya umma dhidi ya wakimbizi, kupatiwa hifadhi katika nchi ya tatu, kama ilivyo kwa Rahaf, hufanyika kwa idadi ndogo sana ya wakimbizi milioni 25.4, hususan wale walio hatarini zaidi kama vile watoto.

UNHCR imesema suala la Rahaf lilishughulikiwa kwa kiwango cha udharura kwa kuzingatia uharaka wa masaibu yaliyokuwa yanampata.

Taarifa ya UNHCR inasema hivi sasa Rahaf yuko njiani kuelekea Canada.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud