Wakimbizi tukikirimiwa tunarejesha fadhila kwa jamii:Bahati, Micheline na Agnes

Kambini Kakuma
UN/Esperanza Tabisha
Kambini Kakuma

Wakimbizi tukikirimiwa tunarejesha fadhila kwa jamii:Bahati, Micheline na Agnes

Wahamiaji na Wakimbizi

Kutana na wakimbizi Bahati Hategekimana kutoka Rwanda, Micheline Muhima kutoka Uganda na Agnes Mude kutoka Sudan Kusini ambao wote walikuwa wakiishi kwenye kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya, lakini sasa kupitia mradi wa majaribio wa kuthamini mchango wa wakimbizi EMPP, unaoendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, mjini Pictou na serikali ya Canada watatu hao si wakimbizi tena bali ni wafanyakazi wa huduma ya jamii kwenye kituo cha Glen Haven Manor kilichopo jimboni Nova Scotia nchini Canada. 

Bahati, mmoja kati ya wasichana hao watatu waliobahatika kuchukuliwa na kuajiriwa kama wafanyakazi wa kudumu wa  huduma kwenye kituo cha kuhudumia wazee jimboni Nova Scotia baada ya kufaulu usaili wakiwa kambini Kakuma , anasema anahisi fursa hiyo aliyopata si hisani bali amestahili kwani ameifanyia kazi na anajivunia. 

Jimbo la Nova Scotia nchini Canada mfano wa kuigwa

Jamii ya mjini Pictou jimboni Nova Scotia kwa muda mrefu inakumbatia na kukirimu wakaimbizi ikiwapa malazi na chakula lakini sasa inaenda mbali zaidi kwa kubaini ujuzi wa wakimbizi na kuwapatia ajira ikishirikiana na serikali, UNHCR na wadau wengine kupitia mradi wa majaribio wa EMPP. 

Sarah Wiseman Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa mji wa Pictou anasema “Tulichokifanya kwa waajiri wa eneo hili ni kuwafahamisha kwamba kuna kundi lingine la waajiriwa wenye ujuzi ambalo wanaweza kuliangaliawatu hao wana ujuzi, uzoefu na eimu wanayohitaji lakini wamejikuta ni wakimbizi”. 

Lengo la mradi huo ni kubaini wakimbizi wenye ujuzi na kuwaunganisha na waajiri ambao wanawafanyia usahili popote walipo na kuwapa ajira inayowasafirisha hadi Canada kufanya kazi. 

Maisha mapya Canada kutoka ukimbizi Kakuma

Baada ya kuwasili Nova Scotia Bahati, Micheline na Agnes walipewa nyumba na wameanza maisha mapya. Micheline Muhima aliwasili na mwanae mdogo mwenye umri wa miaka miwili na ana matumaini makubwa” Najua mustakabali utakuwa bora, kwa familia yangu na watoto wangu na kwangu mimi kwani nataka kuwa na ujuzi fulani wa kazi.” 

Agnes Mude anasema maisha yake yamebadilika tangu alipofika Canada na anashindwa kuficha furaha yake “Mahali hapa ni pazuri sana, na watu ninaofanya nao kazi ni wakarimu sana hali inayonifanya kuhisi ninakubalika.” 

Wakimbizi wote hawa watatu wa zamani wanaishukuru sana UNHCR lakini zaidi wanasema wanaamini kwamba jamii zikiwakumbatia wakimbizi basi wakimbizi nao wanarejesha fadhila.