Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwezi mmoja wa vita Ukraine wafurusha zaidi ya nusu ya watoto nchini humo

Watoto wamelazimika kukimbia Ukraine. Pichani ni familia ikiwasili kwenye mji wa Berdyszcze nchini Poland baada ya kuvuka mpaka kutoka Ukraine kukimbia mashambulizi.
© UNICEF/Tom Remp
Watoto wamelazimika kukimbia Ukraine. Pichani ni familia ikiwasili kwenye mji wa Berdyszcze nchini Poland baada ya kuvuka mpaka kutoka Ukraine kukimbia mashambulizi.

Mwezi mmoja wa vita Ukraine wafurusha zaidi ya nusu ya watoto nchini humo

Afya

Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ukitimu mwezi mmoja hii leo, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linasema vita hivyo vimesababisha zaidi ya nusu ya watoto nchini Ukraine kukimbia makwao.

Idadi hiyo ni sawa na watoto milioni 4.5 katika taifa hilo la Ulaya ya Kati linalokadiriwa kuwa na watoto milioni 7.5, imesema UNICEF katika taarifa yake iliyotolewa leo katika miji ya New York, Marekani na Kyiv, Ukraine.

Takwimu hizo zinaonesha kati yao hao waliofurushwa makwao, zaidi ya milioni 1.8 wamekimbilia nchi jirani na waliosalia ni wakimbizi wa ndani. Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell anasema vita hivyo vimesababisha moja ya janga kubwa zaidi la wakimbizi watoto tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia, “hii ni historia yenye kiza ambayo inaweza kuwa na madhara ya kudumu kwa vizazi vijavyo. Usalama, ustawi na fursa ya watoto kupata huduma za msingi viko katika tishio kutokana na ghasia.”

Athari za vita kwa watoto

Kando ya watoto hao kufurushwa, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu, OHCHR inasema tangu kuanza kwa vita tarehe 24 mezi uliopita, watoto 78 wameuawa, na wengine 105 wamejeruhiwa, ingawa inasema takwimu zinaweza kuwa kubwa zaidi.

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani, WHO linazungumzia kuharibiwa kwa miundombinu ya afya na hivyo watoto kushindwa kupata huduma za msingi za afya.

“Huduma za chanjo zimepungua hususan chanjo za polio na surua na hii inaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa yanayoweza kuzuilika,” imesema UNICEF.

Bi. Russel amesema katika wiki chache vita imevuruga watoto Ukraine, “watoto wanahitaji amani na ulinzi wa haraka. Wanahitaji haki zao. UNICEF inaendelea kutoa ombi la sitisho la mapigano haraka iwezekanavyo na ulinzi wa watoto dhidi ya hatari yoyote.”

UNICEF na wadau wanafanya nini?

Ni kwa mantiki hiyo amesema UNICEF na wadau inaendelea kufikia watoto Ukraine na nchi jirani walikokimbilia ili kuwapatia misaada muhimu ya kibinadamu.

Mathalani nchini Ukraine, UNICEF imesambaza vifaa vya matibabu katika hospitali 49 zilizoko kwenye mikoa 9 ikiwemo Kyiv, Kharkiv, Dnipro na Lviv na hivyo kuimarisha huduma za afya kwa wajawazito 400,000, watoto wachanga na watoto.

Halikadhalika inaendelea kusambaza maji saf ina salama na huduma za kujisafi kwenye maeneo ambayo bado yamezingirwa na mapigano.

Hata hivyo UNICEF bado inaomba ulinzi kwa wahudumu wa kibinadamu sambamba na kuondolewa kwa vikwazo vya usafirishaji ili kufikia walengwa katika maeneo yote nchini Ukraine.

Daktari akitembelea kwenye eneo lililo handakini ambako anaficha wagonjwa dhidi ya mashambulizi. Hapa ni katika hospitali ya Wilaya ya Kati huko Brovary, Ukraine
© WHO/Anastasia Vlasova
Daktari akitembelea kwenye eneo lililo handakini ambako anaficha wagonjwa dhidi ya mashambulizi. Hapa ni katika hospitali ya Wilaya ya Kati huko Brovary, Ukraine

Vita imeathiri utoaji chanjo dhidi ya COVID-19

WHO kwa upande wake inasema vita imesambaratisha mfumo wa afya nchini Ukraine, ufikiaji wa huduma za afya una mkwamo, na kuna ongezeko kubwa la mahitaji ya matibabu dhidi ya kiwewe na magonjwa ya muda mrefu.

Katika siku 28 za vita, WHO imethibitisha mashambulizi 64 dhidi ya vituo vya afya na watu milioni 18 wameathirika.

“Kuharibiwa kwa miundombinu ya afya na kuvurugwa kwa mfumo wa usambazajiwa vifaa vya matibabu kunatishia afya ya mamilioni ya watu nchini Ukraine,” imesema taarifa ya WHO iliyotolewa mjini Copenhagen Denmark hii leo.

Daktari akimfunga bandeji mgonjwa aliyejeruhiwa kwenye mapigano yanayoendelea nchini Ukriane.  Hapa ni katika mji mkuu wa Ukraine, Kyiv.
© WHO/Anastasia Vlasova
Daktari akimfunga bandeji mgonjwa aliyejeruhiwa kwenye mapigano yanayoendelea nchini Ukriane. Hapa ni katika mji mkuu wa Ukraine, Kyiv.

Takribani watu milioni 7 ni wakimbizi wa ndani, na waliokimbilia nchi ya Jirani inakaribia milioni 4.
WHO inasema hiyo ina maana raia 1 kati ya 4 nchini Ukriane amelazimika kukimbia makazi yake na kuchochea hali mbaya zaidi kwa wale wenye magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile kisukari, kiharusi.

“Idadi kubwa ya hospitali zimegeuzwa kuhudumia wagonjwa waliojeruhiwa vitani huku nusu ya maduka ya dawa Ukraine yameripotiwa kufungwa. Idadi kubwa ya wahudumu wa afya wamelazimika kukimbia makwao au wanashindwa kufanya kazi,” imesema taarifa hiyo ikinukuu shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji, IOM.

Kama hiyo haitoshi, utoaji wa chanjo dhidi ya COVID-19 na chanjo nyingine za kwenye ratiba umesitishwa. Kabla ya vita takribani watu 50,000 walikuwa wanapatiwa chanjo dhidi ya COVID-19 kila siku. “Kati ya terhe 24 mwezi Februari na tarehe 15 mwezi huu, ni watu 175,000 walipatiwa chanjo hiyo, kiwango ambacho ni cha chini.

WHO imeendelea kutoa huduma licha ya changamoto zilizoko kwenye uwanja huo wa vita.

“Nimeshuhudia kwa macho yangu utoaji wa kipekee wa huduma za kibinadamu katika nchi Jirani na Ukraine, lakini dharura hii bado kabisa kumalizika. Tunatarajia watu wengi zaidi, wanawake na watoto na wazee wenye mahitaji ya kiafya wakiendelea kukimbia katika wiki zijao. Wanaweza kukabiliwa na changamoto za kupata huduma na dawa wanazohitaji, nah ii inaweza kutishia maisha yao,” amesema Dkt. Henri P. Kluge, Mkurugenzi wa WHO kanda ya Ulaya.