Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kadri mashambulizi yanavyoendelea, ndivyo matatizo ya kibinadamu yanaongezeka Ukraine-Griffiths

Martin Griffiths akitoa maelezo kuhusu Ukraine kwa Baraza la Usalama lililokaa New York, Marekani akiwa Geneva.
UN WebTV
Martin Griffiths akitoa maelezo kuhusu Ukraine kwa Baraza la Usalama lililokaa New York, Marekani akiwa Geneva.

Kadri mashambulizi yanavyoendelea, ndivyo matatizo ya kibinadamu yanaongezeka Ukraine-Griffiths

Msaada wa Kibinadamu

Wakati ulimwengu ukishuhudia mashambulizi ya kijeshi nchini Ukraine "kwa hali ya kutoamini na kutisha", Naibu Katibu Mkuu katika Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura, Martin Griffiths amelithibitishia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo Jumatatu kwamba "raia tayari wanalipa gharama". 

Bwana Griffith ameeleza picha ya kiwango cha kutisha cha vifo na majeruhi kwa rai ana pia miundombinu, kukatika kwa upatikanaji wa vitu muhimu na huduma huku kukiwa na kupanda kwa kasi kwa mahitaji ya kibinadamu katika maeneo yaliyoathirika zaidi. 

Amefafanua akieleza kuwa familia zimetenganishwa, wazee na wale wenye ulemavu wamekwama huku mashambulizi ya anga na mapigano katika maeneo ya mijini yakivuruga huduma muhimu, kama vile afya, umeme, maji na vyoo. 

"Hii inawaacha raia bila mahitaji ya msingi ya maisha ya kila siku," amesema mkuu huyo wa misaada ya kibinadamu, na kuzitaka pande zote kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu, kuwaepusha raia kutokana na madhara, na kuepuka kutumia silaha za milipuko katika maeneo yenye wakazi wengi na akaongeza akisema, "kadiri mashambulizi haya yanavyoendelea, ndivyo matatizo ya kibinadamu yavyoongezeka kwa raia". 

Athari kwa watoto na wanawake 

Watoto watakosa shule na kukabiliana na hatari kubwa zaidi ya madhara ya kimwili, kufurushwa, na msongo wa kihisia; na wanawake, ambao mara nyingi wameathiriwa bila uwiano na migogoro, watakuwa katika hatari kubwa zaidi ya unyanyasaji wa kijinsia, kwa muujibu wa Bwana Griffith.  

“Na ikiwa uchumi utadorora, mahitaji ya kibinadamu yataongezeka zaidi, na kusababisha athari mbaya zaidi ya mipaka ya Ukraine.” Amesema Griffith.  

Wanajitahidi 

Bwana Griffith amebainisha kuwa licha ya kuongezeka kwa uwepo wa wafanyakazi wa huduma za kibinadamu za Umoja wa Mataifa wanaofanya kazi usiku kucha nchini Ukraine, kwa siku tatu zilizopita, mapigano yanayoendelea na ukosefu wa hakikisho kutoka kwa pande za mzozo kwamba harakati za kibinadamu zitalindwa "zimezuia kwa kiasi kikubwa" operesheni za misaada ya kibinadamu. 

"Leo, mahitaji yetu makubwa ya kibinadamu ni huduma za dharura za matibabu, ikiwa ni pamoja na huduma za afya ya uzazi, dawa muhimu, maji salama ya kunywa na kujisafi, pamoja na makazi na ulinzi kwa waliokimbia makazi." amesema Bwana Griffiths.