Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umeme, mabomu ya kutengwa ardhini na uchumi vipewe kipaumbele Ukraine: Griffiths

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya  kuratibu misaada ya dharura, OCHA, Martin Griffiths akiwa Kherson katika ziara yake ya siku nne nchini Ukraine.
© UNOCHA/Saviano Abreu
Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA, Martin Griffiths akiwa Kherson katika ziara yake ya siku nne nchini Ukraine.

Umeme, mabomu ya kutengwa ardhini na uchumi vipewe kipaumbele Ukraine: Griffiths

Msaada wa Kibinadamu

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya  kuratibu misaada ya dharura, OCHA, Martin Griffiths amehitimisha ziara yake ya siku nne nchini Ukraine na kutaja mambo makuu matatu muhimu ya kupatiwa kipaumbele kuwa ni mosi; kurejesha umeme kwenye makazi, pili kutegua mabomu yaliyoko kwenye makazi ya watu na tatu, ni kuchechemua shughuli za kiuchumi ili maisha yaweze kuendelea na kwamba Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia.  

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kyiv bwana Griffiths amekumbusha kwamba mashirika ya misaada ya kimataifa yametoa msaada kwa watu karibu milioni 14 tangu kuanza kwa vita nchini Ukraine. 

Ameongeza kuwa mashambulizi mpya ya Urusi dhidi ya miundombinu ya nishati ya Ukraine yanaweza kusababisha kuzorota kwa hali ya kibinadamu na kufanya watu wapya kuyahama makazi yao.  

Huko Bucha, Ukraine, wakaazi wanajiandaa kukabiliana na majira ya baridi bila umeme.
OHCHR/Anthony Headley
Huko Bucha, Ukraine, wakaazi wanajiandaa kukabiliana na majira ya baridi bila umeme.

Mambo hayo matatu muhimu 

Akisisitiza kuhusu umuhimu wa nishati ya umeme amesema “Nilishangaa sana jinsi umeme ulivyo lango la kila kitu kingine. Bila umeme, hakuna joto. Hali ya hewa inazidi kuwa baridi. Bila umeme, hakuna huduma za matibabu, hakuna usafiri, hakuna mwanga, hivyo umeme ni muhimu sana.” 

Kastika kipengele cha pili cha umuhimu wa kutegua mambomu ya kutegwa ardhini mkuu huyo wa misaada ya kibinadamu amesema “Niliambiwa, kwa mfano, kwamba kuna takriban ekari nusu milioni za ardhi ya kilimo huko Kherson pekee ambazo zinahitaji kusafishwa. Huwezi kuanzisha upya uzalishaji wa kilimo nchi humu bila kuondoa mabomu hyaliyotegwa ardhini.” 

Na mwisho katika suala la uchechemuzi tena wa uchumi akasema “Hata wakati wa vita, watu wanataka kuona mustakhbali wao, na labda hasa wakati wa vita. Kuanzisha upya vipengele vya ufufuaji wa uchumi wa ndani ni kipaumbele kikuu cha watu. Watu wanataka kurudi kazini. Wanataka watoto wao warejee shuleni, wanataka usafiri wa kwenda kazini,” 

Katika ziara hiyo mbali ya kuzuru mjini mkuu Kyiv pia alipata fursa ya kutembelea hususan miji ya Mykolaiv and Kherson, ambayo hivi karibuni imechukuliwa na vikosi vya jeshi la Ukraine.