Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fainali za FIFA Qatar kutumika kuhamasisha dhidi ya COVID-19

Katika picha hii ya maktaba, Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt Tedros Adhom Ghebreyesus na Rais wa FIFA Gianni Infantino wametia saaini mkataba wa ushirikiano kati ya mashirika hayo mawili ili kuhamasisha maisha ya kiafya kupitia mchezo wa mpira wa miguu kimatai
WHO/Christopher Black
Katika picha hii ya maktaba, Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt Tedros Adhom Ghebreyesus na Rais wa FIFA Gianni Infantino wametia saaini mkataba wa ushirikiano kati ya mashirika hayo mawili ili kuhamasisha maisha ya kiafya kupitia mchezo wa mpira wa miguu kimataifa.

Fainali za FIFA Qatar kutumika kuhamasisha dhidi ya COVID-19

Afya

Kuelekea fainali za kombe la dunia mabara kwa mchezo wa soka zitakazofanyika huko Qatar kuanzia tarehe 4 hadi 11 mwezi huu wa Februari, shirikisho la soka duniani, FIFA na shirika la afya la Umoja wa  Mataifa, WHO wameingia makubaliano kutumia fursa hiyo kusongesha na kuendeleza usawa katika matibabu, chanjo, upimaji na kinga dhidi ya dhidi ya ugonjwa wa Corona au COVID-19.

 

Makubaliano hayo yametangazwa leo mjini Geneva, Uswisi katika mkutano uliohudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus,  Rais wa FIFA  Gianni Infantino na mwanasoka nguli wa kimataifa kutoka Uingereza ambaye sasa ametundika daluga, Michael Owen.

Taarifa ya WHO iliyotolewa Geneva, baada ya makubaliano hayo imesema pande mbili hizo zitawatumia wanasoka nyota kutangaza kupitia televisheni na mabango ya kwenye viwanja ya mpira mpango wa kufanikisha kupatikana kwa haraka mbinu za kukabili COVID-19, ACT uliozinduliwa mwezi Aprili mwaka jana na pia kusihi watu kuvaa barakoa, kuzingatia kuepuka mchangamano na kunawa mikono kwa maji na sabuni na pia vitakatishi.

“Sote tunapaswa kutekeleza wajibu wetu katika vita dhidi ya virusi vya Corona. Tunatoa wito pia kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua pamoja kuhakikisha kuna usawa katika upatikanaji wa chanjo, tiba na vifaa vya upimaji duniani kote,” amesema Bwana Infantino akizungumza kupitia video kabla ya kuanza kwa mashindano hayo ya fainali za FIFA kwa mabara.

Ni kwa kufuata ushauri wa wataalamu wetu wa afya ndio tutaweza kutokomeza vitisho vya COVID-19- Gianni Infantino, Rais wa FIFA

Kwa upande wake Dkt. Tedros ameshukuru FIFA na wachezaji kwa kusaidia kuhamasisha umma juu ya mbinu za kuokoa maisha ambazo watu wote wanaweza kuzifuata ili kujiepusha na Corona.

“Usawa ni msingi wa soka na aina zote za michezo, na hili pia ni muhimu linapokuja suala la afya. Kanuni za kukabili COVID-19 ni rahisi: watu wote walio hatarini kuambukizwa COVID-19 wanapaswa kuwa na haki sawa ya kupata chanjo ya kuokoa maisha, matibabu na vipimo. Katika miezi 9, dunia imeweza kutengeneza chanjo 3 thabiti dhidi ya Corona. Lakini lengo letu sasa ni kuhakikisha upatikanaji sawia wa chanjo hizi kwa watu wote,”  amesema Mkurugenzi Mkuu huyo wa WHO.

Ubia huo mpya wa FIFA na WHO utapazia zaidi sauti ujumbe kwa wakazi wa dunia kupitia video za uhamasishaji zitakazotangazwa wakati wa mashindano hayo huko Qatar.

Katika video hizo, manahodha wa timu zinazoshiriki michuano hiyo wanasisitiza hatua muhimu kwa kila mtu kufuata ili kukabili na kutokomeza virusi vya Corona kwa kuwa makini kwenye mikono, viwiko, nyuso, umbali, dalili, barakoa na kuhakikisha madirisha ya nyumba walimo yako wazi.

“Ni muhimu tusisahau kuwa afya lazima iwe jambo la kwanza,”  amesema Rais wa FIFA akiongeza “ni kwa kufuata ushauri wa wataalamu wetu wa afya ndio tutaweza kutokomeza vitisho vya COVID-19 na natoa wito kwa kila mtu kufuata hatua hizo kila siku ya maisha yao. Ushauri huu siyo tu unakulinda wewe pekee bali pia na wapendwa wako na wale walio karibu na wewe.”

Video hizo zenye ujumbe pamoja na kuchezwa wakati wa michuano huko Qatar, zitachapishwa pia katika mitandao mbalimbali ya kidijitali ya FIFA na WHO kwa ushirikiano na mashirika ya utangazaji duniani.
Timu zinazoshiriki ni 6  mwaka huu zikiwemo zile za washindi wa makombe ya vilabu na nchi mwenyeji wa mashindano ambayo ni Qatar. 

Timu hizo ni Bayern Munich, Al Ahly, Palmeiras, Ulsan Hyundai, Tigres UNANL na Al Duhanil.
Michuano hiyo awali ilikuwa ifanyike mwaka jana lakini iliahirishwa kutokana na janga la COVID-19.