Virusi vya Corona kama dharura ya afya ya umma:Taarifa za UN News Kiswahili
Mlipuko uliripotiwa mara ya kwanza Wuhan China Desemba 31, 2019

Ukurasa huu unaleta pamoja taarifa kuhusu muongozo kutoka kwa Shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO na Umoja wa Mataifa kuhusu mlipuko wa sasa wa virusi vya corona au COVID-19, ambavyo viliripotiwa mara ya kwanza Wuhan, China mnamo Desemba 31, 2019. Tafadhali tembelea ukurasa huu kupata taarifa za kila siku. WHO inafanya kazi kwa karibu na wataalam wa kimataifa, serikali na wadau kupanua ujuzi wa kisayansi kuhusu virusi hivi vipya, kutokana na jinsi vinavyosambaa na athari zake  na kutoa ushauri kwa nchi na watu, kuhusu hatua za kuchukua kwa ajili ya kulinda afya na kuzuia kuenea kwa mlipuko.

UN yatumia teknolojia kuhakikisha kazi inaendelea huku ikilinda afya ya wafanyakazi na wadau wake

Kufuatia kuendelea kuenea kwa maambukizi ya virusi vya Corona, COVID-19, Umoja wa Mataifa umeimarisha harakati za kulinda wafanyakazi wake na watu wengine wote wanaotumia ofisi zake kote ulimwenguni huku ukihakikisha kuwa shughuli zake zinaendelea ikiwemo kutekeleza majukumu yake ya kupatia msaada wale wenye uhitaji.