Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yatumia teknolojia kuhakikisha kazi inaendelea huku ikilinda afya ya wafanyakazi na wadau wake

Mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa akisafisha mikono kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York.
UN Photo/Loey Felipe
Mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa akisafisha mikono kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York.

UN yatumia teknolojia kuhakikisha kazi inaendelea huku ikilinda afya ya wafanyakazi na wadau wake

Afya

Kufuatia kuendelea kuenea kwa maambukizi ya virusi vya Corona, COVID-19, Umoja wa Mataifa umeimarisha harakati za kulinda wafanyakazi wake na watu wengine wote wanaotumia ofisi zake kote ulimwenguni huku ukihakikisha kuwa shughuli zake zinaendelea ikiwemo kutekeleza majukumu yake ya kupatia msaada wale wenye uhitaji.

Katika barua pepe yake kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa kuelekea mwishoni mwa juma, Katibu Mkuu António Guterres, amesisitiza kuwa, “shirika hilo liko wazi likiendelea kufanya kazi zake. Kazi yetu itakuwa inafanyika kutoka kona mbalimbali kwa kutumia teknolojia mbalimbali.”

Amewaambia wafanyakazi kuwa ni lazima tutekeleze wajibu wetu kwa kuonyesha mshikamano na wale walio hatarini zaidi; wazee, wagonjwa na wale wasio na huduma ya uhakika ya afya.

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa kuna umuhimu wa kupunguza “idadi ya uwepo wetu kwenye jengo la makao makuu ya Umoja wa Mataifa kwa kutekeleza mpango wa kufanyia kazi kutoka nyumbani. Wafanyakazi ambao ni lazima wawepo jengoni ili kuweza kutekeleza majukumu yao muhimu hao watalazimika kuwepo.”

Tweet URL

 

Bwana Guterres amesema kuwa suala la kupunguza zaidi idadi ya wafanyakazi kwenye jengo litatathminiwa baada ya wiki tatu.

Ameongeza kuwa wafanyakazi kwenye makao makuu ya UN wataendelea kutoa huduma muhimu kwa ofisi nyingine za Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswisi, Nairobi, Kenya na Vienna, Austria na pia kwenye ofisi nyingine masihnani na kwamba michakato mingine yoyote na serikali inapaswa kuendelea kama vile kazi za Baraza la Usalama.

“Katika siku na wiki zijazo, tutategemea zaidi kila utashi wa mtu wa uwajibikaji na ueledi kuliko wakati wowote ule.”  Amesema Katibu Mkuu kwenye barua pepe  hiyo kwa wafanyakazi akiongeza kuwa “nina imani kubwa na azma ya wafanyakazi ya kuendelea kuhakikisha wako salama huku wakiendelea kutoa huduma kwa wale tunaowahudumia.”

WHO
How to protect yourself against COVID-19

 

Bofya hapa kupata habari zaidi kuhusu virusi vya Corona

Mapema kabla ya kuongezwa kwa muda wa wafanyakazi kufanyia kazi nyumbani, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric, aliwaambia waandishi wa habari jijini New York, Marekani kuwa hofu kubwa ya Katibu Mkuu ni mbili, ambapo mosi ni kuhakikisha kila mtu makao makuu yuko salama, awe mfanyakazi au mgeni na kusaidia jiji la New York, kukabili COVID-19 wakati huu ambapo kirusi hicho kinazidi kusambaa.

Amesema pili ni “ni kuhakikisha kuwa kazi za Umoja wa Mataifa zinaendelea. Tuna walinda amani 100,000 kwenye maeneo ya kulinda amani, makumi ya maelfu ya wafanyakazi wa kibinadamu ambao watahitaji msaada.”

Ameongeza kuwa “naweza kukuhakikishia kuwa iwe ni Bi. Rosemary DiCarlo au Jean-Pierre Lacroix, Mark Lowcock na mameneja wengine wote wamejikita kuona kuwa wanahakikisha kazi inaendelea na msaada unaendelea..”

Bwana Dujarric amesema kuwa wafanyakazi wa misaada mashinani walikuwa na jukumu maalum la kuweka hatua za kuepusha kuenea kwa virusi vya Corona kwa watu walio hatarini zaidi duniani.