Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vifo milioni 9 kutokana na homa ya kichomi vinaweza kuzuilika kwa kuimarisha juhudi-UNICEF

Homa ya kichomi inadai maisha ya watoto zaidi ya 800,000 chini ya miaka mitano kila mwaka. Nchini Nigeria (pichani) watoto walikuwa idadi kubwa zaidi ya wale waliokufa, na wastani wa vifo 162,000 mwaka 2018.
UNICEF/Siegfried Modola
Homa ya kichomi inadai maisha ya watoto zaidi ya 800,000 chini ya miaka mitano kila mwaka. Nchini Nigeria (pichani) watoto walikuwa idadi kubwa zaidi ya wale waliokufa, na wastani wa vifo 162,000 mwaka 2018.

Vifo milioni 9 kutokana na homa ya kichomi vinaweza kuzuilika kwa kuimarisha juhudi-UNICEF

Afya

Vifo milioni 9 vinaweza kuzuilika kwa kuimarisha juhudi za kukabiliana na homa ya kichomi miongoni mwa watoto, na magonjwa mengine kwa mujibu wa  ripoti ya utafiti iliotolewa leo wakati wa kuanza kwa kongamano la kwanza kuhusu homa ya kichomi miongoni mwa watoto mjini Barcelona nchini Uhispania.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema vifo kutokana na homa ya kichomi vinatokea katika nchi masikini zaidi duniani na ni watoto walio tengwa na wenye mahitaji mengi ndio huteseka zaidi.

Kwa mujibu wa makadirio  ya shirika hilo watoto milioni 6.3 walio chini ya umri wa miaka mitano huenda wakafariki dunia kutokana na homa ya kichomi kati ya mwaka 2020 hadi 2030 kulingana na halli ya sasa huku idadi kubwa ya vifo katika muongo mmoja ujao vikitarajiwa kutokea nchini Nigeria watoto milioni 1.4, India 880,000, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, 350,000 na Ethiopia 280,000.

Juhudi za kuingilia kati zinazolenga kuimarisha lishe, kutoa viuavijasumu na kuimarisha utoaji chanjo na  kuongeza idadi ya watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama ni muhimu katika kupunguza hatari ya watoto kufa kutokana na homa ya kichomi na pia kupunguza vifo kutokana na magonjwa mengine kama vile kuhara kunakosababisha vifo milioni 2.1, melengelenge vifo milioni 1.3 na surua vifo 280,000.

Uchafuzi wa hali ya hewa unachangia asilimia 17.5 sawa na karibu kifo kimoja kati ya vitano vya homa ya kichomi miongoni mwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kote ulimwenguni kwa mujibu wa utafiti wa taasisi ya vipimo vya afya na uchunguzi.

Uchafuzi wa ndani kutokana na nishati ya kupika ya mkaa au kuni unasababisha vifo 195,000.

Sababu nyingine zinazochangia katika vifo vya homa ya kichoimi ni utapiamlo, ukosefu wa chanjo na usugu wa dawa za viuavijiasumu.

Homa ya kichomi husababishwa na bakteria, virusi au kuvu na husababisha watoto kuhsindwa kupumua kwani mapafu yao yanakuwa yamejaa usaa na maji. Ugonjwa hui ni moja ya sababu kuu ya vifo na ilisababisha vifo vya watoto laki nane mwaka jana sawa na mtoto mmoja kila sekunde 39.

UNICEF imesema licha ya kwamba baadhi ya aina za homa ya kichomi zinaweza kuzuilika kwa chanjo au kwa viuavijiasumu iwapo inagunduliwa. Hatahivyo mamilioni ya watoto bado hawajachanjwa na mtoto mmoja kati ya watatu wenye dalili hawapati matibabu sahihi.

Kongamano hilo la Januari 29-31 ambalo linaleta pamoja wadau kuhusu afya ya watoto na serikali kutatangazwa aina ya chanjo ya PCV ya bei nafuu na kuchagiza dhamira ya kisiasa kutoka serikali katika nchi zinazobeba mzigo mkubwa kwa ajili ya kuweka mikakati kupungunza vifo kutokana na homa ya kichomi.