Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Homa ya vichomi na utapiamlo ni mtihani mkubwa kwa watoto Yemen-UNICEF 

Kadri mzozo unavyoshika kasi Yemen, raia ndio waumiao zaidi na maisha ya watoto wachanga yako hatarini kama ilivyo pichani kwenye hospitali ya Alsadaqah mjini Aden. IOM imeingilia kati kusaidia.
©UNICEF/Saleh Baholis
Kadri mzozo unavyoshika kasi Yemen, raia ndio waumiao zaidi na maisha ya watoto wachanga yako hatarini kama ilivyo pichani kwenye hospitali ya Alsadaqah mjini Aden. IOM imeingilia kati kusaidia.

Homa ya vichomi na utapiamlo ni mtihani mkubwa kwa watoto Yemen-UNICEF 

Afya

Homa ya vichomi na utapiamlo vimeelezwa kuwa ni moja ya changamoto kubwa kwa afya ya watoto nchini Yemen mbali ya changamoto zingine zinazosababishwa na vita vinavyoendelea, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Katika kituo cha afya cha Al-Hattan wilaya ya Hamdan mjini Sana’a Yemen, watoto wakifanyiwa uchunguzi wa afya zao ikiwemo kupimwa uzito, macho, meno na hata kuhakikisha wamepatiwa chanjo muhimu. Kwa mujibu wa UNICEF mbali ya madhila ya vita homa ya vichomi na utapiamlo vimeendelea kuwa mtihani mkubwa inayochangia vifo vingi vya watoto hususan wa chini ya umri wa miaka 5. Na wazazi wengi wanashindwa kuwapeleka watoto wao kwenye vituo vya afya kutokana na machafuko yanayoendelea.

OM Amirah alimpeleka mwanye katika kituo cha afya cha Al-Hattan tayari akiwa taaban, “Mwanangu alikuwa na homa Kali na alikuwa anaharisha sana, nilimpeleka kwenye kituo cha afya na waligundua alikuwa ameathirika na utapiamlo. Walimpatia matibabu mchanganyiko na sasa anaendelea vizuri.”

 Mtoto wa Amirah ni miongoni mwa mamia ya watoto wanaowasili katika kituo cha afya cha Al-Hattab kila uchao kama anavyoeleza Dkt. Marwan Abdo Mohammed ambaye ni mtaalamu bingwa wa masuala ya watoto kituoni hapo,“Kila siku kituoni hapa tunapokea watoto kati ya 10 na 15 wakiwa na matatizo mbalimbali ikiwemo utapiamlo, homa ya kichomi na wale wanaotaka kupata chanjo. Tunapowapokea watoto cha kwanza tunawaandikisha na kisha tunaangalia ni matibabu gani ambayo mtoto huyo anahitaji.

Kutokana na machafuklo yanayoendelea Yemen kwa muda kituo hiki kilishindwa kutoa huduma lakini  sasa kupitia msaada wa UNICEF kimeanza tena kufanya kazi na kinaweza kutoa huduma mbalimbali kwa mamiaya watoto ikiwemo hewa ya oksijeni ambayo ni muhiumu sana kwa watoto wenye matatizo ya kupungua.

Dkt. Noorsat Rafiki afisa wa afya wa UNICEF nchini Yemen anasema shirika hilo linajitahidi kwa kila hali kuokoa maisha ya watoto nchini Yemen, ’Yemen imekuwa katika hali tete na imeathirika sana na vita kwa miaka mitano iliyopita ambayo vimesababisha mifumo kukaribia kusambaratika na hasa mfumo wa afya na usafi, hivyo UNICEF inajitahidi kuimarisha mifumo hii na kuzuia isisambaratike ili kumfikia kila mtoto kwa huduma muhimu za afya ‘’

 Kwa sasa UNICEF inawahimiza wazazi wote kuhakikisha wanawapeleka watoto kwenye vituo vya afya ili kupimwa na kupatiwa matibabu yanayostahili.