Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vifaa muhimu ili kudhibiti milipuko ya kipindupindu vimewasili nchini Sudan-WHO

Picha ya maktaba ikionesha WHO na wadau wengine walipopeleka msaada wa kudhibiti ugonjwa wa surua katika eneo la West Darful mwezi April 2015 nchini Sudan. Huduma kama hiyo sasa iko katika majimbo ya Sudan Kusini
WHO Sudan
Picha ya maktaba ikionesha WHO na wadau wengine walipopeleka msaada wa kudhibiti ugonjwa wa surua katika eneo la West Darful mwezi April 2015 nchini Sudan. Huduma kama hiyo sasa iko katika majimbo ya Sudan Kusini

Vifaa muhimu ili kudhibiti milipuko ya kipindupindu vimewasili nchini Sudan-WHO

Afya

Shehena ya tani 36 za dawa na vifaa tiba dhidi ya kipindupindu vimewasili mjini Khartoum, Sudan na vinaandaliwa kusambazwa ikiwa ni shemu ya msaada wa shirika la afya duniani WHO kwa Sudan kupambana na mlipuko wa Kipindupindu.

Taarifa iliyochapishwa katika ukurasa wa WHO imeeleza kuwa shehena hiyo imebeba, pamoja na mambo mengine, vifaa vya dharura vya kupima ugonjwa RDTs vipatavyo 5000 kwa ajili ya kuwachunguza wagonjwa waliko katika vituo vya afya na katika maeneo yaliyoko hatarini.

Shehena hiyo pia imebeba dawa zinazoweza kuwatibu watu 2500 walioko katika hali mbaya baada ya kupoteza maji mwilini. Mzigo huo utasambazwa katika vituo vya matibabu kwenye majimbo ya Blue Nile na Sinnar ambako visa vya Kipindupindu vimeripotiwa, pia katika maeneo ya majimbo jirani yaliyoko hatarini kama vile White Nile, Kassala, Gedaref na Khartoum.

Mwakilishi wa WHO nchini Sudan Dkt Naeema Al Gasseerm amesema, “tunakimbizana na muda pamoja na wizara ya afya ya Sudan, mamlaka za serikali na wadau wengine kudhibiti mlipuko na kuzuia vifo zaidi.”

Kwa mujibu wa WHO, hadi kufikia juzi tarehe 24 Sptemba 2019, jumla ya visa 184 vimeripotiwa, vikiwemo visa 128 katika jimbo la Blue Nile na visa 56 katika jimbo la Sinnar. Wizara ya afya ya Sudan imeripoti vifo nane vinavyohusaiana na kipindupindu ambapo visa 6 ni katika jimbo la Blue Nile na vifo viwili kutoka jimbo la Sinnar.