WHO na Sudan wachukua hatua kudhibiti mlipuko wa kipindupindu Khartoum

6 Novemba 2019

Shirika la afya ulimwenguni, WHO, linashirikiana na wadau wake kusaidia kuepusha kuenea zaidi kwa mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu kwenye jimbo la Khartoum nchini Sudan ikiwemo mji mkuu Khartoum.

Mwakilishi wa WHO nchini Sudan Dkt. Naeema Al Gasseer amenukuliwa katika taarifa iliyotolewa leo mjini Khartoum akisema kuwa hatua ya shirika hilo inafuatia ombi la Waziri wa Afya wa Sudan Dkt. Akram Eltoum.

Amesema kinachofanyika sasa ni kuhakikisha kuwa watu wote wanaoshukiwa kuugua Kipindupindu wanatambuliwa na kupatiwa matibabu haraka, na watu wengine waweze kujikinga na ugonjwa huo.

Dkt. Al Gasseer amesema, hatari ya kusambaa kwa kipindupindu ni kubwa mno na iwapo hatua sahihi hazitachukuliwa, madhara makubwa yanaweza kutokea kwa kuzingatia kuwa zaidi ya watu milioni 8 wanaishi jimbo la Khartoum ambako mifumo wa afya ya umma imesambaratishwa na janga la kiuchumi pamoja na mafuriko ya hivi karibuni.

Hadi tarehe 3 mwezi huu wa Novemba, Wizara ya Afya nchini Sudan imeripoti wagonjwa 332 wanaoshukiwa kuwa na kipindupindu, na idadi kubwa iko kwenye majimbo ya Blue Nile na Sennar. Tarehe 19 mwezi uliopita wa Oktoba, wagonjwa wawili wa kipindupindu walithibitishwa jimboni Khartoum.

Tayari Wizara ya Afya na WHO wamebainisha maeneo  yaliyo hatarini zaidi kupata kipindupindu kwenye jimbo la Khartoum na hatua hiyo itasaidia kuweka mipango bora zaidi ya kudhibiti mlipuko kwenye maeneo hayo ikiwemo vitongoji vya Sharq Elnil na Ombada.

Vituo navyo vyapatiwa vifaa vya matibabu

Mwakilishi huyo wa WHO Sudan amesema pia ili kuhakikisha kuwa vituo vya afya na vile vya kutibu kipindupindu vina vifaa vya kutosha kubaini na kutibu wagonjwa, Who imesambaza dawa za tiba zinazoweza kutosha wagonjwa 400 na vipimo 500 vya kubaini haraka kipindupindu.

Halikadhalika wanasaidia kuanzisha vituo viwili vya kutibu kipindupindu kwenye vitongoji vya Ombada na Bahri na kuvipatia pia dawa za tiba, vifaa vya matibabu na vya kupima.

Shirika hilo pia linapatia mafunzo mapya kwa wahudumu 271 wa afya na wasaidizi kutoka vitongoji 7 ili waweze kutambua jinsi ya kubaini na kusimamia harakati dhidi ya ugonjwa huo.

Elimu kwa jamii kuhusu kipindupindu

Dkt. Al Gasseer amekumbusha kuwa msingi wa kudhibiti kuenea kwa kipindupindu ni jinsi gani jamii inaweza yenyewe kujikinga kwa kunywa maji safi na salama, chakula salama na kuepuka kujisaidia maeneo ya wazi, kunawa mikono na kutambua kile cha kufanya wakati wanapoona dalili za awali za ugonjwa huo.

Kwa mantiki hiyo hivi sasa WHO na Wizara ya Afya ya jimbo la Khartoum wanashirikiana na waelimishaji wa afya 1700 wa kike na wakiume na wafanyakazi wa kujitolea ambao watakuwa na dhima adhimu ya kuelimisha jamii juu ya kujikinga na kipindupindu kwa kuwa na huduma za usafi na kujisafi na kuweka mazingira safi.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud