Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Marekani chunguzeni chanzo cha kifo cha mtoto mhamiaji: Mtaalam

Wakimbizi na wahamiaji kutoka Venezuela.
©IOM/Amanda Nero
Wakimbizi na wahamiaji kutoka Venezuela.

Marekani chunguzeni chanzo cha kifo cha mtoto mhamiaji: Mtaalam

Wahamiaji na Wakimbizi

Mtaalam Maalum wa Umoja wa Mataifa ameelezea wasiwasi wake mkubwa  kufuatia tukio la mtoto wa kike mhamiaji kutoka Guatemala  kufariki dunia mikononi mwa maafisa wa uhamiaji wa  Marekani.

Katika taarifa iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi, mtaalam huyo maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya haki za wahamiaji, Felipe Gonzales Morales, ametaka ufanyike uchunguzi wa kina wa kifo cha mtoto huyo Jakelin Amei Caal aliyekuwa na umri wa miaka 7.

Halikadhalika ametaka Marekani ikome kushikilia watoto kwa misingi ya hadhi yao ya uhamiaji.

Ingawa kumekuwa na maelezo tofauti kuhusu hali ya kiafya yam toto huyo, Bwana Morales amesema ni suala lisilo na ubishi wowote kuwa Jakelin alifariki dunia akiwa mikononi mwa  wafanyakazi wa idara ya Marekani ya mipaka na uhamiaji baada ya kuvuka mpaka kutoka Mexico na kuingia  Marekani akiwa na baba yake na kundi kubwa la wahamiaji.

Mtaalam huyo Maalum amesema, “wakuu wa Marekani ni lazima wahakikishe kuwa uchunguzi wa kina, tena ulio huru unafanyika kuhusiana na kifo hicho.

Ametaka pia familia yake ipewe haki ya kisheria kwenye mchakato wa kusaka haki ikiwemo uwakilishi wa kisheria kwa lugha ambayo wanaelewa.

Mtaalam huyo pia ameelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu jinsi Marekani inatendea wahamiaji pamoja na maoni ya wananchi wa Marekani kuhusu wahamiaji akisema amewasiliana na serikali ya nchi hiyo kujadili masuala kadhaa na ni matumaini yake kuwa wanaweza kuwa na mashauriano ya kina kupatia suluhu suala hilo.

Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa, tafadhali jisajili na pia unaweza kupakua apu ili kuweza kusikiliza wakati wowote popote ulipo.