Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwekezaji ugenini wapungua, nchi zinazoendelea hazikuathirika- UNCTAD

Meli ya mizigo ikiwa na shehena yake kwenye bandari ya Ningbo, China
IMO
Meli ya mizigo ikiwa na shehena yake kwenye bandari ya Ningbo, China

Uwekezaji ugenini wapungua, nchi zinazoendelea hazikuathirika- UNCTAD

Ukuaji wa Kiuchumi

Uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni, FDI, ambao hutajwa kama kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi duniani, umeporomoka kwa zaidi ya asilimia 40 katika nusu ya kwanza yam waka huu wa 2018.

Hii ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD iliyotolewa hii leo.

Kiwango hicho ambacho ni sawa na dola bilioni 470 kimekumba nchi tajiri zaidi duniani hususan zile za Ulaya na Ameriak Kaskazini.

Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi wa UNCTAD anayehusika na uwekezaji James Zhan amesema “kwa ujumla taswira nzima ya kifedha duniani ina kiza. Uwekezaji wa  moja kwa moja wa kigeni ni muhimu kwa sababu hupatia nchi fursa ya kupata mitaji ya nje, teknolojia, somo na mchango wa kodi.”

Kwa mujibu wa UNCTAD, hali hii ya sasa inatokana na marekebisho ya mfumo wa kodi yaliyofanywa na Marekani, marekebisho ambayo yanahamasisha kampuni kubwa nchini humo kurejesha nyumbani mapato yao, hususan kutoka nchi za Ulaya Magharibi.

Urasimishaji wa sekta isiyo rasmi ni moja ya mbinu za kukuza uchumi wa nchi
IFAD
Urasimishaji wa sekta isiyo rasmi ni moja ya mbinu za kukuza uchumi wa nchi

“Mwanzoni mwa mwezi wa Januari, tulihadharika kuwa kuna hisa zenye thamani ya dola trilioni mbili zikiwa kama fedha taslimu au mapato yaliyowekezwa tena, fedha ambazo zimetokana na mapato yaliyohifadhiwa nje ya Marekani na marekebisho  ya kodi yanaweza kuchochea kurejesha angalau nyumbani baadhi ya mapato  hayo,” amesema Bwana Zhan akiongeza kuwa “na  hakika hili linafanyika. Tumeshuhudia FDI kutoka Marekani mwaka jana ilitoka dola bilioni 147 hadi dola hasi bilioni 247 mwaka huu.”

FDI NA MIRADI INAYOJALI MAZINGIRA

Kwa mujibu wa Zhan, masuala mengine yaliyosababisha kampuni za Marekani kurejesha faida zao nyumbani ni kutokuwa na taarifa za kina kuhusu marekebisho hayo ya mfumo wa kodi na kutofahamu mustakhbali wa athari za mzozo wa kibiashara kati ya Marekani na China.

Hata hivyo licha ya kupungua kwa FDI bado kuna ongezeko la asilimia 42 la uwekezaji kwenye miradi inayojali mazingira ambayo thamani yake imefikia dola bilioni 454.

Halikadhalika ripoti imesema kwa nchi zinazoendelea, anguko hilo la FDI halikuwa na athari kubwa kwa kuwa limepungua kwa asilimia 4 pekee.

AFRIKA NAYO JE? NCHI GANI INAONGOZA KWA FDI

Kwa bara la Afrika, uwekezaji wa kigeni umepungua kwa asilimia 3 na kufikia dola bilioni 18 katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, ingawa Afrika Kusini imepata mafanikio zaidi kwenye kuvutia mitaji ambayo imeongezeka kwa asilimia 40.

“Hii inadokeza kwamba nchi hii inashuhudia kurejea upya kwa kiwango cha uwekezaji baada ya kudorora miaka iliyotangulia,” imesema ripoti hiyo ikifafanua kuwa Misri imesalia nchi inayoongoza barani Afrika kwa kupokea FDI.