Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola bilioni 4.4 si haba kwa wasyria

Katika mji wa Al-Taqba nchini Syria, mtoto mwenye umri wa miaka 12 akiwa na rafiki zake wakitembea kando mwa gari lililolipuliwa kutokana na mapigano nchini humo. Watoto hawa hawafahamu familia zao ziko wapo na UN inahaha kuwasaidia.
©UNICEF/Souleiman
Katika mji wa Al-Taqba nchini Syria, mtoto mwenye umri wa miaka 12 akiwa na rafiki zake wakitembea kando mwa gari lililolipuliwa kutokana na mapigano nchini humo. Watoto hawa hawafahamu familia zao ziko wapo na UN inahaha kuwasaidia.

Dola bilioni 4.4 si haba kwa wasyria

Msaada wa Kibinadamu

Baada ya mashauriano na mazungumzo na pia kusikia kauli kutoka kwa wawakilishi wa wananchi wa Syria, wahisani wamefungua pochi zao na kuchangisha fedha kukuwamua wananchi hao ambao mustakhabali wao uko mashakani.

Huko Brussels, Ubelgiji hii leo wahisani wamechangia jumla ya dola bilioni 4.4 kwa ajili ya wakimbizi wa Syria na ukanda wa Mashariki ya Kati.

Mchango huo ni kutoka kwa wahisani 36 na umetangazwa mwishoni mwa mkutano wa pili wa kimataifa kuhusu Syria ulioandaliwa kwa pamoja na Umoja wa Mataifa, UN na Muungano wa Ulaya, EU.

Fedha hizo zitaelekezwa siyo tu kwenye mahitaji  ya kibinadamu bali pia miradi ya kuwawezesha wasyria kujikwamua kimaisha.

Mkuu wa ofisi ya UN ya kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA, Mark Lowcock akizungumza mwishoni mwa mkutano huo amesema, “ahadi hizi ni mwanzo mzuri. Katika dunia ya sasa tungalipenda kuchangisha fedha zaidi na tunatarajia kupata fedha zaidi mwaka huu. Fedha hizi ambazo wahisani wametupatia kwa ukarimu zinaleta tofauti kubwa sana katika maisha ya wasyria ambao wamenasa kwenye janga la kutisha.”

Jamii ya kimataifa pia imethibitisha kupatikana kwa dola bilioni 3.4 kwa ajili ya kufadhili misaada ya kibinadamu na maendeleo kwa wasyria kwa mwaka 2019 na 2020.

 

Chai na kunde ndio mlo wetu

JANGA LA SYRIA NDIO LIMETAPANYA RAIA WENGI

Mzozo wa Syria ndio unaongoza duniani kwa kutawanya raia ambapo watu milioni 13.1 wanahitaji misaada ya kibinadamu na ulinzi ndani ya nchi yao huku wengine zaidi ya milioni 5.6 wakiwa wamesaka hifadhi nje ya nchi.

Wakimbizi hao wa Syria wamesaka hifadhi Uturuki, Lebanon, Jordan, Iraq na Misri.

UN inasema wakimbizi wa ndani nchini Syria wanahitaji dola bilioni 3.6 ilhali wale walioko nje ya nchi yao wanahitaji dola bilioni 5.6.