Nchini Syria watoto hawajui maana ya amani- UN

27 Julai 2018

Zaidi ya watoto 7,000 wamepoteza maisha yao au wamejeruhiwa na kuachwa na ulemavu wa kudumu kutokana na mgogoro unaoendelea nchini Syria.

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto walio kwenye mizozo, Virginia Gamba, amesema hayo leo akihutubia Baraza la Usalama la umoja huo jijini New  York, Marekani.

Bi. Gamba amesema watoto hao wamenyanyaswa kwa muda mrefu na pande zote kinzani kwenye mzozo huo uliodumu kwa miaka nane sasa na watoto hao hawafahamu amani ni nini.

 (SAUTI YA VIRGINIA)

Huu ndio wakati kwa watoto wa Syria  kuwa na imani katika mustakbala wao na pia kujifunza  kuhusu amani ni nini. Na huu ndio wakati kwa watoto hao kujeresha utoto wao waliopokonywa na huu ndio wakati wa watoto kukomesha kitendo cha wao kuwa waathirika.”

Bi Gamba amesema kuwa  tangu  mwanzo wa mgogoro huo  mwezi Machi mwaka 2011, Umoja wa Mataifa umethibitisha  visa vya zaidi ya watoto 7,000 kuuawa au kuachiwa umelavu wa kudumu.

 

Viginia Gamba,Mwakilishi maalum wa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto walio kwenye mizozo.
UN Photo/Rick Bajornas
Viginia Gamba,Mwakilishi maalum wa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto walio kwenye mizozo.

Amesisitiza kuwa idadi hiyo  ni ile tu ambayo imethibitishwa akiongeza kuwa ripoti ambazo hazijathibitishwa zinatoa idadi ya watoto walioathiriwa katika mgogoro huo kufika  20,000.

 Amesema kuwa watoto hao wameteseka na kunyanyaswa kupindukia ikiwemo makwao, kijamii, shuleni, vituo vya kizuizi na pia katika kambi za wasio na makazi.

Bi. Gamba amesema haki za watoto zilikiukwa akirejelea mfumo wa ufuatiliaji na utoaji wa taarifa uliopitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, mwaka 2005 au MRM.

Mfumo huo ulioangazia maeneo sita ya ukiukwaji wa haki za watoto kwenye maeneo yenye mizozo ulianza kutekelezwa mwaka 2013 nchini Syria baada ya baraza hilo kupitisha azimio.

Maeneo hayo ni kuua na kujeruhi kunakoacha ulemavu wa kudumu, , kusajili watoto vitani, unyanyasaji wa kingono, utekaji wa watoto, kushambulia shule au hospitali na pia kuwanyima msaada wa kibinadamu.

 

Mark Lowcock,Naibu katibu Mkuu wa ofisi ya  umoja wa Mataifa ya kuratibu  misaada ya binadamu, OCHA, katika mkutano wa kuhusu hali nchini Syria
UN Photo/Rick Bajornas
Mark Lowcock,Naibu katibu Mkuu wa ofisi ya umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya binadamu, OCHA, katika mkutano wa kuhusu hali nchini Syria

Wajumbe pia walipata maelezo kutoka kwa mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu  misaada ya binadamu, OCHA, Mark Lowcock ambaye aliweka bayana hali ya kibinadamu nchini Syria akisema nchi ihyo imekumbwa na vita karibu kila mahali.

(SAUTI YA MARK LAWCOCK)

“  Tangu Novemba 2017 idadi ya  watu wanaohitaji msaada wa kibinadamu maeneo ya  Aleppo na Idlib  imeongezeka kwa takriban watu  600,000  na kufikia jumala ya watu   milioni 4.2. Na nusu ya watu  hao wanahitaji msaada wa haraka kutokana na kutokuwa na makazi, chakula, maji pamoja na mahitaji mengine muhimu.”

Pia amebaini kuwa  ombi la mwaka huu la  msaada kwa Syria limepata pesa chache  na kuongeza kuwa kasi ya kukabiliana na matukio sehemu hiyo inategemea  msaada kutoka nchi wanachama na wahisani.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter