Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tukinyamaza nani awasemee watoto wa Syria?- Blok

Watoto wakiteka maji huko Douma, mji ulioko kwenye eneo la Ghouta Mashariki, nje kidogo ya mji mkuu wa Syria, Damascus.
UNICEF/Bassam Khabieh
Watoto wakiteka maji huko Douma, mji ulioko kwenye eneo la Ghouta Mashariki, nje kidogo ya mji mkuu wa Syria, Damascus.

Tukinyamaza nani awasemee watoto wa Syria?- Blok

Msaada wa Kibinadamu

Syria! Syria! Syria! Bado ni kizungumkuzi,  maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yanapitishwa lakini wahusika ni kama kusema "wameweka pamba masikioni."

Iwapo Baraza la Usalama halitatumia mamlaka yake ya kuleta amani Syria nani ataweza kufanya hivyo?

Ni moja ya kauli lukuki zilizotamalaki wakati wa kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichokutana leo kutathmini utekelezaji wa azimio lake namba 2401 la kutaka sitisho la mapigano nchini Syria.

Zaidi ya mwezi mmoja tangu kupitishwa kwa azimio hilo bado hali ya usalama na kibinadamu si shwari.

Umoja wa Mataifa na wadau wake wanakumbwa na mkwamo siyo tu kwenye kuwasilisha misaada ya kibinadamu, bali pia kuwahamisha wagonjwa mahututi.

Mark Lowcock, Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na misaada ya dharura, OCHA akihutubia kwa njia ya video aliweka bayana hali huko Ghouta na Idlib.

Hapa ni Kafar Batna, kijiji kilichopo kwenye viunga vya mji mkuu wa Syria, Damascus na watoto wanakusanya matawi ya miti yatakayotumiwa kwa kuni.i.
UNICEF/Amer Al Shami
Hapa ni Kafar Batna, kijiji kilichopo kwenye viunga vya mji mkuu wa Syria, Damascus na watoto wanakusanya matawi ya miti yatakayotumiwa kwa kuni.i.

(Sauti ya Mark Lowcock)

“Kwa ujumla wadau wa kibinadamu bado wanahaha kupata ruhusa endelevu kwenye eneo hilo. Halikadhalika wakimbizi wa ndani kutoka wilaya ya Afrin bado wanapata vikwazo kufika Aleppo, Na linalotupa hofu zaidi ni ruhusa ya kuhamisha wagonjwa mahututi ili wapate huduma mahsusi za matibabu mjini Aleppo. Vifo vinne vimeripotiwa kutokana na wagonjwa kukosa matibabu sahihi.”

Akahoji kwa mara nyingine tena.

(Sauti ya Lowcock)

Bwana Rais, azimio namba 2401 lilipitishwa zaidi ya mwezi mmoja sasa. Nasihi nyote chukueni hatua azimio liwe halisia. Licha ya ugumu wowote Umoja wa Mataifa na wadau wake umeazimia kufuatilia kwa faida ya wasyria.”

Rais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Machi ni Uholanzi ambapo Waziri wake wa Mambo ya Nje Stef Blok ndiye aliongoza kikao hicho.

Bwana Blok alionyesha picha za watoto wa Syria ambao angalau wao waliweza kukimbia nchi hiyo na sasa wanaishi Uholanzi akisema wao walibahatika.

Alihoji vipi kwa wale waliosalia Syria?

(Sauti ya Stef Blok)

“Nini mustakhbali wa watoto walio kwenye picha niliyoonyesha. Je siku moja wataweza kurejea Syria. Kama ilivyo kwa watoto wote, nao wanatamani maisha ya kawaida, utulivu na usalama. Mimi mwenyewe ni mzazi na nadhani siko peke yangu kwenye Baraza hili. Picha za watoto walioathirika kwa vita lazima zinamgusa kila mtu. Licha ya tofauti zote baina yetu, angalau tuwe na jambo la pamoja, imani ya kulinda watoto lazima ipatiwe kipaumbele.”

Na ndipo akaweka bayana.

(Sauti ya Stef Blok)

“Ni wajibu yetu kurejesha uhalali wa baraza hili. Ni juu yetu kuhakikisha kuna mchakato wa kisiasa ambamo kwamo wasyria na wadau wote wanawakilishwa. Na ni wajibu wetu kumaliza chuki na kurejesha utu na ubinadamu kwa wananchi wa Syria.”

Tarehe 15 Machi 2018 familia za eneo la Beit Sawa huko Ghouta Mashariki nchini Syria wakisubiria mabasi ya kuwahamishia maeneo mengine salama huko Hamourieh.
UNICEF/Sanadiki
Tarehe 15 Machi 2018 familia za eneo la Beit Sawa huko Ghouta Mashariki nchini Syria wakisubiria mabasi ya kuwahamishia maeneo mengine salama huko Hamourieh.

Hali ni mbaya zaidi huko Ghouta Mashariki na Idlib. OCHA inasema kuwa tangu tarehe 9 mwezi huu zaidi ya watu 80,000 wamekimbia Ghouta.

Kama hiyo haitoshi, zaidi ya watu elfu 50 wanaishi kwenye makazi duni yaliyojaa kupita kiasi.