Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi ya anga yaua watoto na walimu nchini Myanmar

Watoto wanyanyua mkono kujibu swali darasani katika kituo cha masomo cha UNICEF kambini Cox's Bazar, nchini Bangladesh.(Maktaba Julai 8, 2019)
© UNICEF Patrick Brown
Watoto wanyanyua mkono kujibu swali darasani katika kituo cha masomo cha UNICEF kambini Cox's Bazar, nchini Bangladesh.(Maktaba Julai 8, 2019)

Mashambulizi ya anga yaua watoto na walimu nchini Myanmar

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya watoto UNICEF limeeleza kusikitishwa na vifo vya wanafunzi wanne na walimu wawili vilivyotokea siku ya jumatatu tarehe 05 Februari 2024 baada ya mashambulizi ya anga katika shule mbili huko jimboni Kayah, mashariki mwa nchi ya Myanmar. 

Taarifa iliyotolewa leo na Mwakilishi wa UNICEF kanda ya Asia Mashariki na Pasifiki Deborah Comini imesema watoto waliofariki walikuwa na umri wa kati ya miaka 12 na 14. 

“UNICEF inalaani vikali mashambulizi yoyote dhidi ya shule na maeneo ya kusomea, ambayo lazima yawe maeneo salama kwa watoto.” Amesema Bi. Comini na kuongeza kuwa “Mashambulizi dhidi ya shule ni ukiukaji mkubwa wa haki za watoto na sheria za kimataifa za kibinadamu.”

Watoto zaidi ya 100 walikuwa shuleni wakati wa mashambulizi hayo na kwamba watu wengi zaidi wamejeruhiwa.