Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Warohingya 5,000 wapoteza makazi baada ya kambi yao kuteketezwa kwa moto

Moto uliozuka huko Cox’s Bazar, Bangladesh, Rohingya, umewaacha maelfu bila makao.
© UNHCR/Sahat Zia Hero
Moto uliozuka huko Cox’s Bazar, Bangladesh, Rohingya, umewaacha maelfu bila makao.

Warohingya 5,000 wapoteza makazi baada ya kambi yao kuteketezwa kwa moto

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesikitishwa na kitendo cha wakimbizi wa rohingya 5,000 wakiwemo watoto 3,500 kupoteza makazi yao baada ya moto mkubwa kuwaka kwenye kambi namba 5 ya makazi ya wakimbizi ya Cox’s Bazaar nchini Bangladesh. 

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo Dhaka, mji mkuu wa Bangladesh inasema moto huo uliwaka jana Januari 7, 2024 na kwamba hakuna ripoti zozote za vifo na zaidi ya yote hadi sasa hakuna taarifa zozote kuhusu chanzo cha moto huo. 

UNICEF inasema ingawa hivyo takribani watoto 1,500 hawatakuwa na pahala pa kusomea kwani maeneo 20 ya kujifunzia yameteketezwa kwa moto. “Tunavyotathmini uharibifu uliotokea, UNICEF na wadau watajenga mahema ya muda kuwezesha watoto kujifunza wakati madarasa kamilifu yanajengwa,” imesema taarifa hiyo. 

Kwa sasa UNICEF na wadau wanafanya kazi mchana na usiku kusadia watoto waliokumbwa na kiwewe pamoja na familia zao baada ya tukio hilo la moto. 

“Hebu tukumbuke, ha watoto tayari wamekimbia ghasia na kiwewe. Kwa hiyo kuna umuhimu tena wa dharura kwa mamlaka za Bangladesh, Umoja wa Mataifa na wadau wengine kuwapatia mahitaji ya dharura wale walio hatarini zaidi ili watoto wote wawe salama, wawe na afya na walindwe,” imesema UNICEF kwenye taarifa yake. 

UNHCR nayo yazungumza 

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR nalo limeungana na wadau wengine kusaidia manusura wa moto huo. 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani hii leo, msemaji wa Umoja wa Mataifa Florencia Soto Nino amesema takribain makazi 800 yameteketezwa kwa moto huo pamoja na maenoe mengine 120 zikiwemo shule, misikiti na vituo vya afya. 

Kwa sasa, wakimbizi ambao makazi yao yameungua, wamesaka hifadhi kwenye vituo vya kijamii kambini Cox’s Bazaar na wanapatiwa misaada ya dharura kama vile chakula. 

Mamlaka za Bangladesh na UNHR wanaratibiana na shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji, IOM na wadau wengine kusaidia wakimbizi hao wa Rohingya waliopoteza mali na makazi.