Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yapokea msaada wa $Mil 5.4 kusaidia wakimbizi wa Rohingya

Familia moja ya Rohingya inapokea chakula chao cha kila mwezi kutoka WFP.
© WFP/Sayed Asif Mahmud
Familia moja ya Rohingya inapokea chakula chao cha kila mwezi kutoka WFP.

WFP yapokea msaada wa $Mil 5.4 kusaidia wakimbizi wa Rohingya

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP limepokea msaada wa dola milioni 5.4 kutoka serikali ya Japan kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi wa Rhohingya ambao wanakabiliwa na ufinyu wa ufadhili kwa ajili ya chakula na mahitaji mengine muhimu. 

Mwaka jana 2023, kupungua kwa ufadhili wa wafadhili kulilazimisha WFP kupunguza mgao wa chakula kila mwezi kwa wakazi wote wa Rohingya katika kambi ya Cox's Bazar kutoka dola 12 kwa kila mtu kwa mwezi hadi dola 10 mwezi Machi, kisha hadi dola 8 mwezi Juni. 

Akiishukuru serikali ya Japan kwa msaada huo wa fedha zitakazotumika kwa ajili ya chakula cha kuokoa maisha Mwakilishi wa WFP nchini Bangladesh Dom Scalpelli akiwa mjini Dhaka amesema “wakati wanatiwa moyo na ongezeko kiasi la mgao wa chakula, lakini bado njaa na viwango vya utapiamlo katika kambi vinaonesha hitaji la dharura (la Msaada) ili kurejesha mgao wa chakula kikamilifu.”

Kwa upande wake Balozi wa Japan Kiminori Iwama amesema Msaada huu ni ishara tosha ya kuonesha dhamira isiyo yumba ya Japan katika kutoa misaada ya kibinadamu na kwamba “Msaada huu tulioutoa utaenda kushughulikia mateso ya njaa na utapiamlo yanavyowakabili wanajamii wa Rhohingya na kuchangia katika lengo pana la kustawisha utulivu na amani.”

Tunaomba Msaada zaidi

WFP imesema inategemea Japan na jumuiya nyingine za wafadhili kuendeleza usaidizi wao muhimu ili kuhakikisha kwamba wanaweza kukidhi, angalau, mahitaji ya msingi ya chakula na lishe ya Warohingya hadi waweze kurejeshwa makwao salama.

Kutokana na Msaada kutoka kwa wafadhili, kuanzia tarehe 1 Januari, 2024 WFP imerejesha mgawo kwa dola 10 kwa kwa kila mtu kwa mwezi. 

WFP inahitaji ufadhili mwingine wa dola milioni 38 ili kurejesha mgao huo kikamilifu - sasa ni dola za Marekani 12.5 kwa kila mtu kwa mwezi.

Hofu iliyopo

Kwas asa kinachotia wasiwasi zaidi ni kuongezeka kwa ghasia na ukosefu wa usalama katika kambi, pamoja na biashara haramu ya binadamu. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR liliripoti kuwa karibu wakimbizi 4,500 wa Rohingya walianza safari za baharini mwaka 2023, hili ni ongezeko kubwa kuliko miaka iliyopita.