Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hospitali Sudan zaomba usaidizi

Hospitali Sudan zaomba usaidizi

Pakua

Vita nchini Sudan ambayo sasa imedumu kwa zaidi ya siku 100 imeshuhudia zaidi ya watu milioni 3 wakiyakimbaia makazi yao kwenda kusaka hifadhi katika miji mingine pamoja na nchi Jirani. 

Video ya shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi UNFPA inaanza kwa kuonesha chupa cha upasuaji ambako mjamzito amefanyiwa upasuaji na kujifungua salama huko katika mji Port Sudan jimboni Red Sea mashariki mwa nchi ya Sudan.

Hapo awali, hospitali hiyo ilikuwa ikipokea wajawazito 300 mpaka 450 wanaojifungua kwa njia ya kawaida na wale wanaohitaji upasuaji walikuwa takriban 300 kwa mwezi. 

Daktari Randa Osman ni Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo ya Wazazi ya Port Sudan anasema “Idadi ya sasa ni kubwa zaidi kwa sababu ya ongezeko la watu wanaokimbilia katika jimbo hili.” 

Dokta Randa anaendelea kwa kusema wajawazito na watoto wachanga wanakabiliwa na ufikiaji finyu wa huduma muhimu za afya. 

“Hospitali hii ya kujifungulia ndio pekee iliyopo katika mji huu na inatoa huduma za dharura za uzazi, uangalizi baada ya kujifungua na upasuaji. Hospitali imekuwa ikipokea idadi kubwa ya wagonjwa na mzigo wa kazi umeongezeka mara mbili. Watendaji wetu wanafanya kazi bila kuchoka kuwahudumia wakimbizi wanaokaa katika makazi ya muda ya wakimbizi.” 

Daktari huyu anahitimisha kwa kueleza kile wanachohitaji? 

“Tunahitaji vifaa tiba zaidi kwakuwa idadi ya wagonjwa ni zaidi ya mara mbili. Na pia tunahitaji kuongeza juhudi ili kukabiliana na hitaji hili kubwa linalozidi kuongezeka.”

Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi UNFPA linafanya kila juhudi kwa kushirikiana na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa na wadau kuhakikisha wanawasaidia watu wote wenye uhitaji.

Audio Credit
Thelma Mwadzaya
Audio Duration
2'41"
Photo Credit
UNFPA Video