Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita hii ifike mwisho, wakulima tumeumia sana – Mkulima Ukraine

Vita hii ifike mwisho, wakulima tumeumia sana – Mkulima Ukraine

Pakua

Mwishoni mwa mwezi huu wa Februari tarehe 24, utatimia mwaka mmoja tangu uvamizi wa sasa wa Urusi kwa Ukraine. Nchini Ukraine, moja ya sekta zilizoathiriwa sana na vita hii ni kilimo Anold Kayanda anamwangazia mkulima mmoja katika mkoa wa Odesa kusini magharibi mwa nchi.

“Mkasa huu mbaya ulioikumba nchi yetu umeathiri nyanja zote za kilimo”, ni mkulima Volodymry Varbanet akishika mbegu za alizeti alizozalisha na anaongeza akisema, “shughuli zote za kilimo zilichelewa kwa sababu hatukuweza kwa wakati kuuza mazao yetu ya kutoka mwaka jana.” 

Mkulima huyu akionekena mwenye masikitiko anatembea katika shamba lake kwa masikitiko anasema kwamba walipanda alizeti, shayiri na ngano lakini vyote imekuwa hasara kutokana na vita baada ya Urusi kuamuru majeshiyake kuishambulia Ukraine tarehe 24 Februari mwaka jana 2022.

“Hili ni shamba la hekta 10 ambapo tulipanda mbegu za alizeti. Watu wanaogopa kuja kazini. Kombora limeanguka kilomita 15 kutoka eneo hili hivi karibuni. Kombora jingine ambalo liliharibiwa angani lilianguka kwenye kiwanja upande mwingine kama kilomita 10 au 12 kutoka hapa.”

Ingawa chini ya makubaliano yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa, wakulima wa Ukraine wanaweza sasa kusafirisha mazao yao kupitia katika bahari nyeusi kwenda katika eneo jingine la ulimwengu ikiwemo Afrika, kwa Volodymry ndoto yake ni moja tu,

“Nina ndoto moja tu hivi sasa kama walivyo raia wengine wa Ukraine na wakulima wa Ukraine. Ninatamani vita hii ifike mwisho mapema iwezekanavyo. Ninafikiri kila kitu kitakuwa sawa.” 

Audio Credit
Anold Kayanda
Audio Duration
1'48"
Photo Credit
© OCHA/Matteo Minasi