Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu yasalia ndoto kwa watoto wa nchi za Afrika ya Kati na Afrika Magharibi

Elimu yasalia ndoto kwa watoto wa nchi za Afrika ya Kati na Afrika Magharibi

Pakua

Zaidi ya watoto milioni 1.9 wamelazimika kukatisha masomo yao maeneo ya Afrika magharibi na Kati kwa sababu ya ongezeko la mashambulizi na vitisho vya kikatili dhidi ya elimu katika ukanda huo, imesema ripoti mpya ya shrikia la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF iliyotolewa leo Ijumaa. ARnold Kayanda na ripoti kamili.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo,  kufikia mwezi juni mwaka huu wa 2019 shule 9,222 zilifungwa nchini Burkina Faso, Cameroon, Chad, Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mali, Niger na Nigeria kwa sababu ya ukosefu wa usalama hii ikiwa ni mara tatu zaidi ya idadi iliyoripotiwa mwishoni mwa mwaka 2017.

Ikipatiwa jina la Elimu hatarini magharibi na Afrika ya kati, ripoti  inaonya kuwa vitendo vya kulengwa kwa maksudi kwa shule, watoto na walimu kunakoshuhudiwa katika ukanda huo, kunawanyima watoto haki yao ya kusoma na kuwaacha wao na jamii zao katika mazingira ya hofu kwa ajili ya maisha yao na mustakabali wao.

Sauti hiyo ni ya miongoni mwa watoto ambao wamejikuta katika hali kama hiyo ya kutokuwepo shuleni naye ni  Clarisse akiwa nchini Cameroon.

Video ya UNICEF inamuonyesha Clarisse akiwa na mdogo wake akitizama mto.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF, Petri Gornitzka akizungumzia ripoti hiyo amesema, “mashambulizi ya kulenga na yasiyokoma dhidi ya mifumo ya elimu ambao ni msingi wa amani na maendeleo yamewacha giza kwa watoto, familia na jamii kote ulimwenguni.”

Mtoto Clarrisse ameshuhudia mashambulizi hayo na anasema, wanateketeza shule, wanateketeza maeneo ambako watu wanatembea, wanateketeza nyumba za watu, wanateketeza watu wakiwa ndani ya nyumba, wanateketeza kila sehemu.

Ukosefu wa usalama katika maeneo ya kaskazini magharibi na kusini magharibi nchini Cameroon umesababisha shule 4,400 kufungwa katika maeneo hayo na zaidi ya shule 2,000 zimefungwa nchini Burkina Faso, pamoja na shule 900 nchini Mali kwa sababu ya ongezeko ya ukatili katika nchi hizo.

Kaitka ukanda wa Sahel katikati, Burkina Faso, Mali na Niger zimeshuhudia ongezeko mara sita zaidi ya kufungwa kwa shule kwa sababu ya mashambulizi na vitisho vya ukatili katika kipindi cha miaka miwili kutoka 512 Aprili 2017 hadi 3,005 mwezi Juni mwaka huu wa 2019. Nchi nnw zilizoathirika na janga katika bonde la ziwa Chad ni Camerron, Chad, Niger na Nigeria ambako viwango vimesalia vya juu kati ya 981 hadi 1,054 katika ya mwisho wa mwaka 2017 hadi Juni 2019.

UNICEF inafanya kazi na mamlaka za elimu na jamii kwa ajili ya kusaidia njia mbadala kwa ajili ya fursa za kupata elimu ikiwemo vituo vya jamii vya elimu, shule kupitia radio, teknolojia ya kufundisha na kusoma na miradi ya kidini.

UNICEF inatoa pia vifaa kwa walimu wanaofanya kazi katika maeneo hatarishi na pia msaada wa kisaikolojia kwa watoto wa shule wanaochwa na makovu ya ukatili.

Watoto walioathirika na mzozo magharibi na Afrika kati wanajumuisha mtoto 1 kati ya 4 kote ulimwenguni wanaohitaji msaada wa kibinadamu ikiwemo elimu na huduma zingine za kuwawezesha kusoma.

UNICEF na wadau wametoa wito kwa serikali, vikosi vilivyojihami na pande husika kwenye mzozo na jamii ya kimatiafa kuchukua hatua kusitisha mashambulizi na vitisho dhidi ya shule, wanafunzi na kuunga mkono elimu kwa kila mtoto katika ukanda huo.

Kufikia Agosti 12 kuna pengo la ufadhili la asilimia 72 wa kusaidia program za watoto.

Audio Credit
Grace Kaneiya/Arnold Kayanda
Audio Duration
2'9"
Photo Credit
UNICEF/Ashley Gilbertson