Wahamiaji vigori wa Nigeria wanakabiliwa na unyanyasaji wa kingono Italia-IOM

Wahamiaji vigori wa Nigeria wanakabiliwa na unyanyasaji wa kingono Italia-IOM

Pakua

Kuna ongezeko kubwa na wahamiaji wasichana vigori wanaowasili Ulaya sanjari na ongezeko la ukatili wa kingono unaohusishwa na uhalifu wa kupangwa.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya matokeo ya utafiti wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita shirika hilo linasema limeshuhudia karibu ongezeko la asilimia 600 la waathirika wa usafirishaji haramu wa binadamu wakiwasili Italia kwa njia ya bahari.

Mwaka 2014 takribani wasichana 1,400 walivuka bahari ya Mediterranea na kuingia Italia , na idadi hiyo imeongezeka na kufikia zaidi ya 11,000 mwaka jana. IOM inasema suala lingine la kusikitisha ni kwamba umri wa wasichana hao unazidi kuwa mdogo kila mwaka. Flavio Di Giacomo ni afisa wa IOM

(SAUTI YA FLAVIO DI GIACOMO)

"Lakini tatizo ni kwamba hawatambui ni unyanyasaji wa kiasi gani watakaokabiliana nao, wakati mwingine hata hawaelewi ukahaba ni nini kwa sababu ni wadogo sana, wamepumbazika sana na hawana ufahamu wowote wa kile watakachokwenda kukabiliana nacho."

IOM inatoa wito kwa wasichana hao wa Nigeria kupelekwa kwenye makazi salama mara tu wanapowasili Italia, lakini ni vigumu kuwashawishi waombe msaada kwa sababu mara nyingi wanasafiri na mtu ambaye anawakabidhi kwa magenge ya wahalifu.

Photo Credit
Mfanyakazi wa IOM akikutana na mhamiaji.(Picha:IOM/2017)