Zeid atoa kauli sakata la kidiplomasia dhidi ya Qatar

Zeid atoa kauli sakata la kidiplomasia dhidi ya Qatar

Pakua

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein amezungumzia sakata la kidiplomasia dhidi ya Qatar akitaka hatua zichukuliwe haraka ili kuepusha kuzorota zaidi kwa haki za binadamu.

Kamishna Zeid amenukuliwa akisema kuwa hivi sasa mvutano huo uliosababisha Falme za kiarabu, Misri na Bahrai kukata uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi na Qatar, umesababisha athari kwa maelfu ya wanawake, wanaume na watoto kwa misingi tu ya kwamba ni raia wa moja ya nchi zinazohusika na mzozo huo.

Amesema ingawa Bahrain, Falme za kiarabu na Misri wamechukua hatua kushughulikia masuala ya kibinadamu kwa raia wenye uraia pacha, bado hiyo haitoshi kushughulikia shida zote.

Yaelezwa kuwa Falme za kiarabu na Bahrain zinatishia kuwafunga jela na kuwatoza faini watu wanaoionea huruma Qatar ambapo Zeid amesema hali hiyo ni ukiukwaji wa haki.

Ametaka suluhu isakwe haraka kupitia mashauriano na kuepusha vitendo vyovyote vitakavyozorotesha ustawi wa watu.

Photo Credit
UN Photo - Jean-Marc Ferre