Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita na migogoro ya muda mrefu ni kikwazo katika kutokomeza njaa:FAO

Vita na migogoro ya muda mrefu ni kikwazo katika kutokomeza njaa:FAO

Pakua

Uhakika wa chakula na viwango vya lishe Mashariki ya mbali na Afrika Kaskazini vimedorora kwa haraka katika miaka mitano iliyopita , vikitishia hatua zilizopigwa kabla ya 2010 ambapo hali ya lishe duni, kudumaa, matatizo ya upungufu wa damu na umasikini vilikuwa vinapungua, imesema ripoti mpya ya shirika la chakula nakilimo FAO iliyotolewa Jumatatu.

Ripoti hiyo “Mtazamo wa kikanda wa uhakika wa chakula Mashariki ya mbali na Afrika Kaskazini” imebaini kwamba kuzorota huko kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na kusambaa na ukubwa wa mizozo na pia migogoro ya muda mrefu kama vita vya Syria.

Utafiti wa FAO unaonyesha kwamba kutokuwa na uhakika wa chakula miongoni mwa watu wazima ktika kanda hiyo kunakaribia asilimia 9.5 kwa mwaka 2014-2015, hiyo ikiwakilisha takriban watu milioni 30.

Ripoti inasema mbali ya vita vya Syria idadi ya watu wenye uhaba wa chakula na wakimbizi wa ndani inaongezeka Iraq na Yemen.

Pia imeongeza kuwa uhaba wa maji na mabadiliko ya tabia nchi ni changamoto kubwa sana katika kutokomeza njaa, kuwa na uhakika wa chakula, kuboresha lishe na kuchagiza malengo ya maendeleo endelevu SDG’s ifikapo 2030.

Photo Credit
Picha: FAO/Giulio Napolitano