Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ufadhili wa haraka unahitajika huku takriban watoto 300,000 wakikabiliwa na utapiamlo mkali kusini mwa Afrika

Wanawake wakiwa wanarejea nyumbani wakipita katika eneo ambao limeathirika vibaya na ukame Gwembe Valley Zambia
© UNICEF/Karin Schermbrucke
Wanawake wakiwa wanarejea nyumbani wakipita katika eneo ambao limeathirika vibaya na ukame Gwembe Valley Zambia

Ufadhili wa haraka unahitajika huku takriban watoto 300,000 wakikabiliwa na utapiamlo mkali kusini mwa Afrika

Afya

Ukame mkali ambao umeathiri maeneo makubwa ya Kusini mwa Afrika na unatishia maisha ya mamia ya maelfu ya watoto katika nchi sita zilizoathiriwa zaidi. Kupitia  taarifa iliyotolewa leo jijini Nairobi, Kenya na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia watoto UNICEF Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika Etleva Kadilli, amesema kuwa zaidi ya watoto 270,000 wanatarajiwa kuugua utapiamlo unaotishia maisha (SAM) mwaka 2024.

Ukame huu umehusishwa na mathara ya  El Niño, ikiwa ni pamoja na mvua kidogo sana, ambazo zimesababisha Lesotho kuwa nchi ya hivi karibuni kutangaza hali ya uhaba wa chakula kitaifa. Nchi nyingine zilizotangaza kukubwa na uhaba wa chakula ni Botswana, Malawi, Namibia, Zambia na Zimbabwe.

"Mahitaji ya kibinadamu yanayowakabili watoto kutokana na El Niño yanahofisha sana," Kuongezeka kwa uhaba wa chakula na utapiamlo, changamoto katika upatikanaji wa maji salama na usafi wa mazingira, pamoja na hatari za milipuko ya magonjwa kama vile kipindupindu ni tishio kubwa. Maelfu ya watoto wako kwenye ukingo wa kupata madhara ya kudumu katika afya na ukuaji wao kwa sababu ya shida inayohusiana na mabadiliko ya tabianchi na onyo hili halipaswi kupuuzwa na jamii ya kimataifa.” ameonya Etleva Kadilli.

Nchini Lesotho, Malawi, Namibia, Zambia, na Zimbabwe, watoto milioni 7.4 wanaishi katika hali ya umaskini wa chakula cha Watoto, ambapo zaidi ya watoto milioni 2 wanakabiliwa na lishe duni ambayo inajumuisha angalau aina  mbili tu za  vyakula. Hali hii imekithiri katika sehemu kubwa za Kusini mwa Afrika kutokana na ukame ikipelekea jamii kupoteza mazao na mifugo kutokana na ukosefu wa malisho na maji.

Watoto wanaoishi katika mazingira magumu ndio wameathiriwa pakubwa zaidi  na majanga ya mabadiliko ya tabianchi Kusini mwa Afrika. Mishtuko hii hupunguza kwa kiasi kikubwa wingi, utofauti, na ubora wa chakula kinachopatikana na  kuathiri vibaya utunzaji wa Watoto. Halikadhalika, inatatiza upatikanaji wa maji safi na salama, na kuwasababishia watoto magonjwa hatarishi ya utotoni ikiwemo kuhara.

Kadili ameongeza kuwa, "kupitia ushirikiano wa kibunifu, mawazo na ufadhili unaojumuisha ushirikishwaji wa jamii kama vile vikundi vya walezi vinavyoongozwa na kina mama vilivyoko nchini Zimbabwe na mpango wa sekta nyingi kwa kiwango kikubwa nchini Zambia, tunaweza kuhakikisha watoto na familia wanaungwa mkono na juhudi endelevu zinazowalinda dhidi ya baadhi ya madhara makubwa ya majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi katika kanda. Kuimarisha mifumo ya kitaifa ya ulinzi wa jamii ni mojawapo ya zana muhimu za UNICEF katika kusaidia familia kujenga uwezo wa kukabiliana na mishtuko ya siku zijazo na kupona kutokana na athari za matukio ya dharura.” 

"Uwekezaji na ubunifu katika kujenga ustahimilivu wa familia na jamii ni muhimu. Mifumo inayobaki imara kwa malengo ya siku zijazo, ikijumuisha mifumo mbalimbali ya chakula, maji safi, huduma za usafi, elimu yenye maudhui ya mabadiliko ya tabianchi, na huduma za afya zinaweza kukabiliana na mathara  mabadiliko ya tabianchi, lazima ipewe kipaumbele, sambamba na kulinda huduma muhimu na mifumo kwa ajili ya watoto ili kuhakikisha ubora na upatikanaji usiokatizwa."

Mbali na uwekezaji katika ustahimilivu, UNICEF imetoa wito wa kuharakisha na kupanua programu za kuokoa maisha kote katika ukanda huo ili kupunguza hatari ya kuongezeka kwa idadi ya watoto wanaokabiliwa na utapiamlo.