UNICEF waomba $Mil 84.9 kusaidia waathirika wa El Nino nchini Zimbabwe
UNICEF waomba $Mil 84.9 kusaidia waathirika wa El Nino nchini Zimbabwe
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limetoa ombi la Msaada wa dola milioni 84.9 kwa ajili ya muitikio wa dharura unaolenga kuwasaidia watoto na wanawake waliaothirika na janga la El Nino nchini Zimbabwe.
Taarifa iliyotolewa leo kutoka Harare nchini Zimbabwe imemnukuu mwakilishi wa UNICEF nchini humo Dlt. Nicholas Alipui akieleza kuwa fedha hizo zitasaidia kutoa Msaada wa kuokoa maisha kwa watu milioni 1.34 ikiwemo watoto 866,000 walio katikati ya janga la kibinadamu lililoathiriwa vibaya ya uhaba wa maji pamoja na upungufu wa chakula.
“Tunatatizwa zaidi na hali mbaya waliyonayo watoto katika hali ya sasa ya dharura. Kuna upungufu wa maji safi na lishe duni na vyote hivi vinaongeza hatari ya utapiamlo na magonjwa ya kuhara miongoni mwa watoto na itaadhiri haki yao ya kupata elimu na kulindwa ndio maana tunahitaji kuharakisha kuja na mikakati ya kuzia vifo katika miezi ijayo” alisema Dkt. Alipui.
Changamoto zilizoletwa na El Nino nchini Zimbabwe zinakuja wakati nchi hiyo ikikabiliwa na dharura za afya ya umma zinazohusiana na kipindupindu na polio, na kuiweka nchi hiyo katika mgogoro tata wa kibinadamu wa pande nyingi.
Ukame unaosababishwa na El Nino unaleta masahibu mengi ya kiafya yanayoathiri watoto, pamoja na milipuko ya magonjwa, magonjwa ya kuambukiza na ya kupumua, na kuongezeka kwa viwango vya utapiamlo. Ukame unaosababishwa na El Nino unaongeza umaskini na mazingira magumu ya kaya na hatari ya kuacha shule, vurugu, na unyanyasaji na unyonyaji dhidi ya watoto.
Uhaba wa maji unatarajiwa kuchangia kuenea kwa magonjwa ya kuhara na magonjwa mengine ya uhaba wa maji kati ya watoto ambayo yanazidishwa na kupungua kwa kinga mwilini kwa watoto kwa sababu ya utapiamlo.
Kwa kuzingatia yote hayo ndioo maana Dkt. Alipui anasema “Ufadhili huo utasaidia kupunguza magonjwa na vifo vya watoto, kuzuia utapiamlo na kutoa matibabu, kuimarisha upatikanaji wa maji, kuhakikisha kuendelea kwa masomo kwa watoto, na kuwalinda watoto dhidi ya unyanyasaji na unyonyaji. Pia itasaidia kuimarisha kaya ili ziweze kukabiliana na mzozo huo,”
Ombi hili lililotolewa leo na UNICEF ni sehemu ya ombi lililotolewa na Umoja na Mataifa pamoja na mashirika mengine ya kimataifa ambalo lilizinduliwa hivi karibuni katika harakati za kusaidia seriali ya zimbabwe kupambana na El Nino.
Ombi la UNICEF linalenga zaidi kuhakikisha kwa kushirikiana na serikali ya Zimbabwe pamoja na wadau wanaendelea kutoa huduma jumuishi kwa watoto na walezi huduma zinazojumuisha masuala ya afya, usafi wa mazingira, maji safi , lishe, elimu na ulinzi wa watoto.