Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wanaendelea kubakwa, kuuawa na kujeruhiwa Sudan, hali ni mbaya : UNICEF

Binti akipatiwa matibabu katika hospitali ya  Khartoum, Sudan
© UNICEF/Mohammed Elibrahimi Isamaldeen
Binti akipatiwa matibabu katika hospitali ya Khartoum, Sudan

Watoto wanaendelea kubakwa, kuuawa na kujeruhiwa Sudan, hali ni mbaya : UNICEF

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF leo limeuelezea mgogoro wa kibinadamu nchini Sudan kama mgogoro uliopuuzwa na ambao madhara yake ni makubwa hususan kwa watoto.

Katika taarifa yake iliyotolewa mjini Geneva Uswis msemaji wa shirika hilo James Elder amesema  mgogoro wa kibinadamu unaolenga  watoto nchini Sudan ni mbaya zaidi duniani huku mengi yanayofanywa dhidi ya watoto yakikosa kuripotiwa.

Elder  akielezea mashambulizi ya hivi karibuni kabisa dhidi ya watoto amesema, “Asubuhi ya Jumamosi timu ya kadanda ya wavulana ilikuwa ikicheza katika eneo rafiki kwa watoto la UNICEF katika Jimbo la Khartoum wakati kombora lilipogonga uwanja wa mpira. Wavulana wawili waliuawa na karibu timu nzima ilijeruhiwa. Nilikutana na watoto hawa, wote wawili wakiwa hospitalini. Nilipowauliza wachezaji wenzake wanatarajia kucheza tena lini, jibu lao lilikuwa moja, asilani!’”

Kuna dharura ya ulinzi  kwa watoto Sudan
UN News/UNICEF
Kuna dharura ya ulinzi kwa watoto Sudan

Ukatili wa kijinsia na kingono

Katika taarifa hiyo Elder pia ameeleza kwa umakini kuhusu viwango vya juu vya ukatili wa kijinsia na kingono dhidi ya wasichana wadogo, akisema kwamba wanawake na wasichana, baadhi yao wakiwa na umri mdogo wa miaka 8, wamebakwa na wengi wanashikiliwa mateka kwa wiki kadhaa."

Aidha amesema kwamba watoto wengi wanaozaliwa baada ya ubakaji huu wanatupwa.

“Maelfu ya watoto wameuawa au kujeruhiwa katika vita ya Sudan. Ukatili wa kijinsia na kuajiriwa kwa watoto vitani kunaongezeka. Na hali ni mbaya zaidi pale ambapo uwepo wa wahudumu wa kibinadamu unaendelea kukataliwa.”

Taarifa hiyo imebaini kwamba watoto milioni 5 wamelazimika kukimbia makazi yao, huku takriban wa watoto 10,000 wakifurushwa kila siku, hali inayofanya Sudan kuwa mgogoro mkubwa zaidi wa watoto kufurushwa duniani.

Kuhusu misaada ya kibinadamu, Elder amesema, “tunapaswa kuwa wazi kabisa, bila ufikiaji salama na usio na vikwazo, hasa  mipakani na katika mipaka ya maeneo ya vita, uamuzi wa mwezi huu wa kutangaza baa la njaa katika sehemu moja ya Sudan unatishia kuenea na kusababisha maafa kwa watoto.”

Kulingana na taarifa hiyo, mbali na Zamzam, maeneo 13 zaidi nchini Sudan, yako katika hatari ya baa la njaa ambayo yanahifadhi watoto 143,000 wanaokabiliwa na aina hatari zaidi ya utapiamlo.

Takriban watu milioni 18 kote nchini Sudan wanakabiliwa na njaa kali.
Nearly 18 million people across Sudan are facing acute hunger.
Takriban watu milioni 18 kote nchini Sudan wanakabiliwa na njaa kali.

Maisha ya watoto yamewekwa rehani

Elder amesema kwamba ingawa wataalamu hawatoi makadirio ya vifo, hali ya sasa inahitaji serikali zenye ushawishi na wafadhili watambue kuwa bila hatua, maelfu ya watoto wa Sudan wanaweza kufa katika miezi ijayo hasa kwa sababu mlipuko wa ugonjwa wowote utaongeza idadi ya vifo.

Kulingana na taarifa hiyo, watoto wa Sudan wanahitaji upatikanaji wa misaada ya kibinadamu bila vikwazo kwa kutumia njia zote, kuvuka mipaka ya maeneo ya vita hasa Darfur, Khartoum, na Kordofan na  uwezo wa kupitia mipakani ya Sudan.

Taarifa hiyo imepongeza kwamba watoto wa Sudan pia watanufaika kama sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu zitaheshimiwa hasa kwa kuongeza ufadhili wa fedha ili kuzuia kuporomoka kwa mifumo muhimu kama kuwalipa wahudumu kwenye vita, kutoa vifaa vya kuokoa maisha, na kudumisha miundombinu muhimu.

Kupitia taarifa hii, UNICEF pia imetoa wito wa mapatano ya haraka ili kuokoa watoto nchini Sudan.

Akimalizia taarifa yake, Elder amesema, “kwa kuipuuza Sudan, na kwa kupuuza mateso makubwa, ina maana pande zinazopigana na jamii ya kimataifa zinaendelea kutokujali  kwa madhila yanayowakabili watoto duniani.”