Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baa la njaa lathibitishwa Darfur Kaskazini nchini Sudan: UN

Watoto na familia za wakimbizi wamekaa katika safu ya mahema ya muda katika kituo cha misaada huko Tambasi, El Fasher, Kaskazini mwa Darfur.
© UNICEF/Mohamed Zakaria Watoto wapumzika kwa kivulini katika kituo cha Tambasi huko El Fasher, Darfur Kaskazini.

Baa la njaa lathibitishwa Darfur Kaskazini nchini Sudan: UN

Amani na Usalama

 

Hatimaye imedhihirika kuwa jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan linakabiliwa na baa la njaa, imesema Kamati ya Tathmini ya Njaa inayohusisha mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau, yakitajwa maeneo yaliyoathirika zaidi kuwa ni kambi ya wakimbizi ya Zamzam kusini mwa El Fasher.

Taarifa inasema ghasia zinazoongezeka nchini Sudan, ambazo zimekuwa zikiendelea kwa zaidi ya miezi 15 sasa, zimezuia kwa kiasi kikubwa ufikiaji wa msaada wa kibinadamu na kusukuma sehemu za Darfur Kaskazini kwenye baa la njaa.

Kwa mujibu wa tathimini “Eneo linatajwa kuwa na baa la njaa pindi mtu mmoja kati ya 5 kwenye familia hana chakula, anakabiliwa na njaa, maskini kupindukia na hivyo kukabiliwa na utapiamlo uliokithiri au kifo.”

Kambi ya wakimbizi wa ndani ya Zamzam iko takriban kilomita 12 kusini mwa mji wa El Fasher na inawakilisha mojawapo ya kambi kubwa zaidi za wakimbizi wa ndani IDP nchini Sudan, ikiwa na takriban ya wakazi wasiopungua 500,000.

Umoja wa Mataifa umesem “Kiwango cha uharibifu unaoletwa na ghasia zinazozidi kuongezeka katika mji wa El Fasher ni kubwa na cha kutisha. Mapigano yanayoendelea, ni makubwa na yamewalazimu wakazi wengi kutafuta hifadhi katika kambi za wakimbizi wa ndani ambapo wanakabiliwa na ukweli mchungu huduma za msingi ni chache au hazipo, na hivyo kuzidisha ugumu wa watu kuhama makazi yao. “

Mvulana mdogo amesimama mbele ya soko katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Al Salaam huko El Fasher, Kaskazini mwa Darfur, Sudan. Nyuma, mwanamke amebeba beseni akipita kwenye makazi ya muda.
© WFP/Leni Kinzli Mvulana akitembea katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Al Salaam Darfur Kaskazini

Zaidi ya watu 300,000 wamekimbia makazi yao

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa Takriban watu 320,000 wanaaminika kuwa wamekimbia makazi yao tangu katikati ya mwezi wa Aprili huko El Fasher.

Takriban 150,000 hadi 200,000 kati yao wanaaminika kuhamia kambi ya Zamzam kutafuta usalama, huduma za msingi, na chakula tangu katikati ya Mei na idadi ya watu katika kambi hiyo imeongezeka hadi zaidi ya nusu milioni katika wiki chache.

Pia imeelezwa kuwa vikwazo vya upatikanaji wa misaada ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na vikwazo vya makusudi vilivyowekwa na pande zinazohusika kwenye mzozo, vimezuia kwa kiasi kikubwa uwezo wa mashirika ya misaada ya kibinadamu kuongeza juhudi zao za kukabiliana na changamoto kwa ufanisi. Vikwazo hivi vimezuia sana utoaji wa misaada muhimu na kuzidisha changamoto ya chakula, na kusababisha baadhi ya kaya kujikuta katika hali ya njaa.

Kama ilivyo kwa njaa yoyote, Umoja wa Mataifa unasema kunakuwa na kuporomoka kwa sekta mbalimbali, na mahitaji ya msingi ya binadamu kama huduma za afya, maji, chakula, lishe, makazi na ulinzi .