Gaza: Wanawake wajawazito walio katika hatari ya kuhama makazi yao, uhaba wa chakula na ugumu wa kupata hospitali
Wakati ripoti za vyombo vya habari zikiripoti kuwa jeshi la Israel litaendelea kuushambulia kwa mabomu Ukanda wa Gaza leo Jumanne, ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya kibinadamu katika eneo la Palestina imeangazia hali mbaya ambayo wanawake wajawazito wanajikuta katika changamoto kubwa, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa ugumu wa kufikia huduma za kuokoa maisha.
Kutokana na mashambulizi dhidi ya vituo vya afya, kuhama mara kwa mara kwa wakazi wa Gaza na ukosefu wa magari ya wagonjwa, maelfu ya wanawake wajawazito wa Palestina wako hatarini.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na misaada ya dharura OCHA "Wanawake wajawazito huko Gaza wanazidi kupata ugumu wa kupata huduma za kuokoa maisha wanazohitaji kutokana na kuhama mara kwa mara, ukosefu wa usalama na mashambulizi dhidi ya vituo vya afya, pamoja na gharama za usafiri na ukosefu wa huduma za magari ya wagonjwa limesema shirika la Amnesty Internationa katika ripoti ya hivi karibuni ya hali Gaza”.
Kujifungua kwa dharura kwenye mahema na bila msaada wa matibabu
Hivi sasa, kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la afya ya uzazi na uzazi UNFPA, huduma ya dharura ya uzazi na huduma ya watoto wachanga inapatikana tu katika hospitali 11 na hospitali za mashambani.
Kufanya mambo kuwa mabaya zaidi, uhaba wa mafuta unatatiza utendakazi wa mashine za kusaidia watoto wanaozaliwa njiti au incubators za watoto wachanga na vifaa vingine muhimu.
"Taarifa zisizo za kawaida zinaonyesha kuwa baadhi ya utoaji wa huduma za dharura unafanyika katika mahema bila msaada wa matibabu," kulingana na UNFPA.
Uhaba wa maji na ukosefu wa dawa za afya ya uzazi pia huwaweka wanawake wajawazito na wanaonyonyesha katika hatari mbalimbali, huku madaktari wakiendelea kutoa taarifa ya ongezeko la watoto wanaozaliwa kabla ya wakati au njiti na wenye uzito mdogo, jambo ambalo ni viashiria vya utapiamlo mkubwa unaochangiwa na msongo wa mawazo, hofu na uchovu.
UNFPA inasema Matatizo yanayoongezeka yanakuja huku Umoja wa Mataifa ukikadiria kuwa takriban wanawake 30,000 wajawazito wanakabiliwa na njaa kali huko Gaza. Wakati huo huo, zaidi ya wanawake 10,000 wako ukingoni mwa njaa na takriban 7,000 tayari wanakabiliwa na hali ya baa la njaa".
Wanawake 155,000 wajawazito na wanaonyonyesha wanahitaji msaada wa dharura
Kwa kuongeza, wanawake 155,000 wajawazito na wanaonyonyesha huko Gaza wanahitaji haraka msaada wa chakula na virutubisho vya lishe, kulingana na UNFPA.
Katika kukabiliana na hali hiyo, washirika na waratibu wa nguzo ya ulinzi na afya wamekuwa wakifanya kazi ili kupanua wigo wa huduma za afya ya uzazi na jinsia, ikiwa ni pamoja na kuajiri, kutoa mafunzo, na kuwapa wahudumu wa afya waliohamishwa kwenye makazi yao, hasa wakunga, kutoa huduma za utunzaji wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua na kuhudhuria utoaji wa huduma za dharura nchini na kwenye vituo vya afya vilivyochaguliwa.
Kwa upana zaidi, Umoja wa Mataifa na washirika wake wa kibinadamu wanaendelea kusaidia familia ambazo zimekimbia kaskazini mwa Gaza hadi maeneo ya kusini.
Timu kutoka OCHA ilitekeleza misheni jana ili kuimarisha operesheni ambapo familia zinawasili eneo la kusini.
Washirika wa misaada ya kibinadamu pia wanasajili watu waliokimbia makazi yao ili waweze kuwapa hifadhi kusini mwa Gaza. Pia wanapanga operesheni katika maeneo ya barabara ya Salahaldeen mashariki mwa Gaza kutathmini mahitaji.
Wiki iliyopita ilikuwa moja ya mauaji makubwa zaidi
kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA “Familia hazipati mahali pa kupata usalama huko Gaza. Operesheni za kijeshi na milipuko ya mabomu ni tishio la mara kwa mara, huku watu waliokimbia makazi yao wakilazimika kuhamia maeneo yenye msongamano mkubwa na yasiyofaa kuishi,"
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limebainisha kuwa Ukanda wa Gaza umekuwa kama jehanamuya hapa duniani.
Aidha, UNRWA imesisitiza kuwa makao yake makuu katika jiji la Gaza "yameharibiwa na kugeuzwa kuwa uwanja wa vita kutokana na kupuuza kwa kiasi kikubwa sheria za kimataifa za kibinadamu na majengo yaliharibiwa kabisa.”
Wiki iliyopita ilikuwa moja yenye matukio mabaya zaidi Gaza tangu kuanza kwa vita. Picha za makao makuu ya UNRWA zinashtua sana, limesema shirikala UNRWA kwenye mtandao wake wa kijamii wa X, na kukumbusha kuwa vituo vya Umoja wa Mataifa sio shabaha na lazima vilindwe wakati wote.
Shule tano zimeathiriwa ndani ya siku kumi
Ikumbukwe kwamba OCHA iliandika kuhusu mashambulio matatu ya Israel yaliyosababisha hasara nyingi, pamoja na mashambulizi mengine matano, katika muda wa siku tatu kabla ya Julai 14, shambulio baya zaidi likiwa ni shambulio la kambi ya wakimbizi wa ndani ya al-Mawasi lililoua Wapalestina 90.
"Katika eneo la Khan Younis, wagonjwa wamejazana kwenye kituo cha Nasser Medical Complex, ambacho tayari kimezidiwa uwezo, kutokana na ukosefu wa vitanda, shuka na vifaa vya usafi," limehitimisha kusema shirika hilo la Umoja wa Mataifa.
Katika siku kumi zilizopita, shule tano zimeathirika. Ya hivi karibuni zaidi ni shule ya UNRWA inayohifadhi familia zilizofurushwa makwao ambayo ndiyo ilikuwa shabaha ya uvamizi wa Israel hapo jana,imesema UNRWA na kukukumbusha kwamba uharibifu na hali ya kukata tamaa vinaendelea bila kikomo katika eneo ambalo hakuna aliye salama.
"Wakati huu mwaka jana, watoto wa Gaza walikuwa wakishiriki katika michezo, mashindano na sanaa katika michezo ya majira ya joto ya UNRWA, mwaka huu wanachuja vifusi na kuomboleza wapendwa wao chini ya shinikizo kubwalinalowatia kiwewe. Vita hivyo vimewapora watoto wa Gaza wa utoto wao," amesema mkuu wa UNRWA Philippe Lazzarini, akibainisha kuwa vituo vya kiraia lazima vilindwe wakati wote na lazima kamwe visitumike kwa madhumuni ya kijeshi au mapigano.