Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shule zaendelea kupigwa mabomu Gaza katika ongezeko la machafuko: UN

Shule iliyolipuliwa na bomu bado inawahifadhi familia moja huko Khan Younis, Gaza.
© UNRWA
Shule iliyolipuliwa na bomu bado inawahifadhi familia moja huko Khan Younis, Gaza.

Shule zaendelea kupigwa mabomu Gaza katika ongezeko la machafuko: UN

Amani na Usalama

Huku kukiwa na ripoti za kuongezeka kwa mashambulizi ya makombora kaskazini, kati na kusini mwa Gaza, mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, amethibitisha leo kwamba kwamba shule zilizogeuzwa makazi ya wakimbizi wa ndani zimepigwa mabomu kutokana na ongezeko la hivi karibuni la mashambulizi.

Philippe Lazzarini ambaye ni mkuu wa  UNRWA amesema, kwenye chapisho like  katika mtandao wa kijamii wa X kwamba "Shule nne zimeshambuliwa kwa makombora katika siku nne zilizopita. Tangu vita kuanza, theluthi mbili ya shule za UNRWA huko Gaza zimepigwa makombora, zingine zililipuliwa, na nyingi zimeharibiwa vibaya,"

Katika taarifa iliyotolewa jana Jumanne, jeshi la Israel lilisema limekuwa likilenga "miundombinu ya kigaidi na waendeshaji wa kigaidi" katika mji wa Gaza.

Chini ya mashambulizi

Jana Jumanne, takriban watu 25 waliuawa baada ya mashambulizi ya Israeli karibu na jengo la shule inayohifadhi watu wa Gaza waliofurushwa mashariki mwa Khan Younis, kusini mwa Gaza, kulingana na mamlaka ya afya ya Gaza

Siku ya Jumamosi, shambulio linguine la makombora lilisababisha vifo vya takriban watu 16 katika shule ya UNRWA huko Nuseirat, katikati mwa Gaza, na kufuatiwa siku moja baadaye na shule katika Jiji la Gaza ambayo iliripotiwa kuwahifadhi mamia ya watu.

Mashambulizi zaidi ya Israeli siku ya Jumatatu yaliripotiwa karibu na shule ya UNRWA huko Nuseirat, kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mawasiliano wa UNRWA Juliette Touma aliyezungumza na UN News.

Hakuna mahali salama

“Hili linakuwa jambo la kawaida, ni katika siku nne zilizopita tumeona shule nne zikishambuliwa,” alisema na kila wakati shule inapopigwa "Makumi ya watu hulipa gharama kwa maisha yao."

Tweet URL

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa ambalo ni shirika kubwa zaidi la misaada ya kibinadamu huko Gaza lilifunga shule zake zote wakati vita vilipozuka tarehe 7 Oktoba mwaka jana kujibu mashambulizi yanayoongozwa na Hamas kwenye maeneo mengi kusini mwa Israel ambayo yalisababisha vifo vya watu 1,250 na zaidi ya 250 kuchukuliwa mateka.

"Tumezigeuza shule nyingi kuwa makazi na wakati fulani tulikuwa na watu milioni moja wanaokaa katika shule zetu," Bi. Touma alieleza, akiongeza kuwa kati ya wahanga wa mashambulizi ya hivi karibuni ya shule, "wengi walikuwa wanawake na watoto”.

Tangu vita kuanza, zaidi ya nusu ya vituo vya UNRWA vingi zaidi ni shule vimeathirika.

"Vingine vililipuliwa kabisa na havifanyikazi tena", Bi. Touma ameendeleam kusema akiongeza kuwa tangu vita kuanza, angalau watoto 600,000 wameshuhudia shule zao zikifungwa.

Kizazi kilichopotea

"Kwa upande wa shule za UNRWA nyingi zilitumika kama makazi, lakini maana yake ni kwamba kama vita hii itaendelea, tuko katika hatihati ya kupoteza kizazi kizima cha watoto," ameendelea kusema.

Ameongeza kuwa “Kadiri watoto wanavyokaa muda mrefu nje ya shule, ndivyo inavyokuwa vigumu kwao kupata fursa ya kuziba hasara ya elimu wanaoipata, na ndivyo hatari ya wao kuangukia kwenye unyanyasaji ikiwa ni pamoja na ajira ya watoto, ndoa za utotoni, lakini pia kuandikishwa katika vikundi vyenye silaha, na kusajiliwa katika mapigano. Kwa hiyo ni kwa ajili ya watoto hao lazima tuwe na usitishaji vita”.

Katika kujibu madai kwamba shule hizo zinatumiwa na wapiganaji wa Hamas au washirika, afisa huyo wa UNRWA amesisitiza kwamba hakuna kituo chochote cha Umoja wa Mataifa kinachopaswa kutumika kwa madhumuni ya kijeshi, kabla ya kurudia wito wa Kamishna Mkuu wa maswali huru na uchunguzi wa haya yoteambayo ni madai mazito.

"Miundombinu ya kiraia, ikiwa ni pamoja na shule, na makazi, na vituo vingine kama vya afya, zahanati, au hospitali, lazima vilindwe wakati wote, ikiwa ni pamoja na wakati wa migogoro," amesisitiza Bi. Touma.

Madhila yanaoongezeka

Katika tukio linalohusiana na hilo, shirika la Umoja wa Mataifa la afya ya uzazi uzazi UNFPA, limeonya kwamba hali ya kibinadamu huko Gaza inaendelea kuwa mbaya zaidi, na "mateso makali sasa yamekuwa ni kawaida.”

Ikinukuu mamlaka ya afya ya Gaza, UNFPA imesema kuwa “karibu Wapalestina 38,000 sasa wameuawa na zaidi ya 87,000 wamejeruhiwa, huku chakula, malazi, afya na rasilimali za kujikimu zikiwa dunisana".

Katika eneo lote Ukanda wa Gaza shirik hilo linasema takriban watu milioni 1.9 wamefurushwa makwao kwa nguvu na mzozo huo mara nyingi zaidi ya mara kadhaa na amri za kuhama zinazotolewa na jeshi la Israeli.

Wakazi wa Gaza wanaishi katika "mahema, makazi yenye msongamano wa watu, au mitaani bila mahitaji ya kimsingi", limesema shirika hilo la Umoja wa Mataifa likionyesha hisia zilizoenea za kukata tamaa kwa watu wenye matarajio madogo ya kurejea nyumbani au kumalizika kwa mzozo.

Vituo vya afya vimeathirika vibaya: WHO

Nalo shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO limesema "Katika kituo cha afya cha UNRWA katika kambi ya wakimbizi ya Jenin, kumeshuhudiwa uharibifu wa miundombinu ya jengo kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara.”

Kwa mujibu wa shirika hilo kliniki hii inahudumia maelfu ya wakimbizi wa Kipalestina ambao wanategemea sana huduma zake za msingi za afya.

Pia WHO imeongeza kuwa kwa kuzingatia ukubwa wake, UNRWA ni muhimu kwa ajili ya kuwasilisha misaada ya kibinadamu inayohitajika na Wapalestina, ikiwa ni pamoja na watu milioni 2.2 huko Gaza na wengine wengi katika Ukingo wa Magharibi.

Taarifa ya  shirika hilo imemalizia kwa kusema kuwa “Wafanyakazi wa misaada wa UNRWA wanaojitolea na wengine lazima waruhusiwe kufanya kazi yao ya kuokoa maisha, bila vikwazo na bila hatari”.