Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yaonya juu ya janga la kiafya linaloshika kasi Congo DRC

Wahudumu wa afya na maafisa wa WHO wakiwa kwenye shughuli za chanjo na uthibiti wa magonjwa kwa wakimbizi katika kambi ya kanyaruchinya wilayani Nyiragongo-Goma
UN News/ Byobe Malenga.
Wahudumu wa afya na maafisa wa WHO wakiwa kwenye shughuli za chanjo na uthibiti wa magonjwa kwa wakimbizi katika kambi ya kanyaruchinya wilayani Nyiragongo-Goma

WHO yaonya juu ya janga la kiafya linaloshika kasi Congo DRC

Afya

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC iko katikati ya janga la kiafya linaloongezeka limeonya leo shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO  na kusisitiza kwamba magonjwa ya milipuko yamezorotesha sana hali nchini humo katika miezi ya hivi karibuni kutokana na ghasia na mafuriko. Kulingana na WHO, DRC imekabiliwa na ongezeko la migogoro na ghasia, na kusababisha watu wengi kukimbia makazi yao, magonjwa kuenea, unyanyasaji wa kijinsia, na kiwewe kikubwa cha akili, haswa mashariki mwa nchi hiyo.

Dkt. Adelheid Marschang, Afisa wa Dharura wa WHO, ameuambia mkutano wa waandishi wa habari wa Umoja wa Mataifa mjini Geneva kwamba "Kutokana na hali hiyo, watu wanakabiliwa na milipuko ya ugonjwa wa kipindupindu, surua, uti wa mgongo, ndui na tauni, yote yakichangiwa na mafuriko makubwa na maporomoko ya ardhi yanayoathiri sehemu kadhaa za nchi hiyo."

Hofu kuhusu lahaja ya mpox

Tangu mwanzoni mwa mwaka, WHO inasema zaidi ya visa 20,000 vya kipindupindu vimerekodiwa, viki katika eneo la Kivu Kaskazini.

Zaidi ya wagonjwa  65,000 wa surau na vifo 1,523 vimeripotiwa, huku idadi halisi ikiwezekana kuwa kubwa zaidi kutokana na kutofuatilia na kuripoti magonjwa kwa kiasi cha kutosha. Wakati huo huo, kkumekuwa na kesi 3,073 za homa ya uti wa mgongo ikiwa ni pamoja na vifo 251vilivyoripotiwa katika  pia zimeripotiwa katika nchi hii ya Maziwa Makuu.

WHO pia imekuwa na wasiwasi juu ya lahaja ya mpox katika miezi ya hivi karibuni katika nchi hii.

Zaidi ya kesi 11,000 zikijumuisha vifo 445 zimerekodiwa, na kukiwa na kiwango cha juu cha vifo vya zaidi ya asilimia 4. Watoto wameelezwa kuathiriwa zaidi na janga hili, na viwango vya juu zaidi vya vifo.

Migogoro ya silaha na watu kuhama makazi yao vimetajwa kuwa ni vichocheo vikuu vya uhaba wa chakula.

Kulingana na ripoti ya hivi karibuni ya uainishaji wa viwango vya uhakika  wa  Chakula IPC, takriban asilimia 40 ya watu ambayo ni saw ana watu milioni 40 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula nchini DRC na, ambapo karibu watu milioni 16 kati yao wako katika hatari ya kutokuwa na uhakika wa chakula.

Msaada wa chakula unasambazwa kwa watu waliokimbia makazi yao mashariki mwa DR Congo.
© WFP/Benjamin Anguandia
Msaada wa chakula unasambazwa kwa watu waliokimbia makazi yao mashariki mwa DR Congo.

Zaidi ya watu milioni 25 wanategemea misaada ya kibinadamu

"Iwapo hakuna hatua za haraka zitachukuliwa kukidhi mahitaji ya msingi nchini DRC, zaidi ya watoto milioni moja watakabiliwa na utapiamlo mkali," ameonya Dkt. Marschang afisa huyo wa WHO.

Ameendelea kusema kuwa hali hii mbaya ya kiafya ni sehemu ya kuzorota kwa hali ya kibinadamu hivi sasa kukiwa na zaidi ya watu milioni 25 wanaohitaji msaada wa kibinadamu, DRC  na kuifanya kuwa sasa ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu wanaohitaji msaada wa kibinadamu duniani.

Takriban watu milioni 7.4 wamekimbia makazi yao, wakiwemo milioni 2.8 Kivu Kaskazini pekee.

Harakati hizi kubwa za watu kuhama zinalemea mifumo ya maji na usafi wa mazingira na kuweka mzigo wa ziada kwa rasilimali chache za watu.

Hata hivyo, ameongeza kuwa chinichini, wasaidizi wa kibinadamu wanapaswa kukabiliana na hali ya usalama inayotia wasiwasi, hasa mashariki mwa DR Congo. Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, WHO imethibitisha mashambulizi 7 kwenye vituo vya afya, ambayo yamesababisha vifo vya watu 3 na kujeruhi 7.

"Kuna uwezekano kwamba mashambulizi hayaripotiwi kutokana na ukosefu wa takwimu," amesema Dkt. Marschang.

Mwaka 2023, WHO ilithibitisha mashambulio 21 ambayo yalisababisha vifo 8 vya wahudumu wa afya na wagonjwa na mtu1 kujeruhiwa.

Huduma za afya za dharura katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro

Wakati nchi hiyo ikikabiliwa na mzozo huu wa janga la kiafya, shirika la Umoja wa Mataifa la WHO limewapatia watu 460,000 huduma za dharura za afya katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro, ikiwa ni pamoja na kukabiliana na mlipuko wa kipindupindu.

"Upatikanaji wa msaada wa kibinadamu unasalia kuwa mdogo kutokana na kuwepo kwa wanajeshi karibu na maeneo ya kambi za wakimbizi wa ndani IDPs, na vituo vya afya, vikwazo vya ukiritimba na vizuizi vya barabarani ambavyo vinatatiza utoaji wa misaada mahali inapohitajika zaidi."

Janga la DRC likizingatiwa kuwa shida iliyosahaulika, WHO inaamini kwamba wasaidizi wa kibinadamu wa Umoja  wa Mataifa hawajaisahau DRC. "Hatuwasahau watu wanaoteseka. Tulienda huko na, pamoja na mazingira magumu zaidi, tulikaa na kutimiza ahadi zetu. Na tumejitolea kuendelea kufanya hivyo. Tunaomba tu, kama shirika lolote la washirika kwamba tuwe na uhakika wa usalama." Amesema afisa huyo wa WHO

Kwa hiyo WHO inataka upatikanaji endelevu na usiozuiliwa wa fursa ya kuwafikia wenye uhitaji na inazitaka pande husika katika mzozo kufanya kazi pamoja kurejesha amani, kama hatua ya kwanza ya kuboresha afya ya akili na kimwili ya watu wote nchini DRC.