Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuelekea uchaguzi Mkuu Sudan Kusini UNMISS yafanya kongamano na vyama vya siasa jimboni Rumbek

Christopher Muchiri Murenga, ni Mkuu wa Ofisi ya Rumbek wa UNMISS nchini Sudan Kusini.
UNMISS
Christopher Muchiri Murenga, ni Mkuu wa Ofisi ya Rumbek wa UNMISS nchini Sudan Kusini.

Kuelekea uchaguzi Mkuu Sudan Kusini UNMISS yafanya kongamano na vyama vya siasa jimboni Rumbek

Amani na Usalama

Wakati nchi ya Sudan Kusini ikijiandaa kwa uchaguzi mkuu wake wa kwanza mwaka huu mwezi Desemba, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS umeendesha kongamano la siku tatu la vyama vya siasa katika mji wa Rumbek ili kujadili masuala ambayo ni muhimu katika maandalizi ya uchaguzi huo. 

Mchakato wa uchaguzi nchini Sudani Kusini unafungamana na utekelezaji wa masharti ya mkataba wa amani uliotiwa saini mwaka 2018 ambao unataka hatua za amani kuchukuliwa si tu katika ngazi ya kitaifa bali majimboni na maeneo yote ya utawala.

Lakini hivi karibuni kumezuka zahma huko katika mji wa Rumbek jimboni Lakes ambako jamii zimejikuta kwenye vurugu za jumuiya mara kwa mara. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana viongozi wa mamlaka za mitaa wakaomba Umoja wa Mataifa kuja kusaidia kuleta amani na umoja kati ya vyama vya siasa vya serikali, vikosi vya usalama na mashirika ya kiraia.

Christopher Muchiri Murenga, ni Mkuu wa Ofisi ya Rumber wa UNMISS, anasema "Sehemu ya kazi yetu muhimu ni kuunga mkono na kusaidia kujenga uaminifu na imani kati ya vyama vya siasa. Wote wamekaa pamoja na kujadili kufungua nafasi ya kiraia na kisiasa katika Jimbo la Lakes, na jambo moja lililotajwa zaidi na watu ni kwamba kongamano hili lisiwe katika manispaa ya Rumbek pekee.”

UNMISS na washirika wa kikanda wanatumaini kuwa kongamano hili na matukio mengine kama haya yatakayo fuata nchini kote yatatengeneza jukwaa la mazungumzo ya wazi na jumuishi kati ya vyama vya siasa na wapiga kura wao kama anavyodhibitisha Waziri wa serikali za mitaa na utekelezaji wa sheria katika jimbo hilo la Lakes bwana Chol Kodowel.

“Tuna jukumu la kuleta utulivu katika jumuiya yetu ili upigaji kura ufanyike katika mazingira ya amani na hilo ni jukumu si kwa serikali ya mtaa peke yake, au jimboni, bali ni jukumu letu sote kama jamii pamoja na wadau wetu.”

Katika ngazi ya kitaifa, vyama vya siasa kwa sasa vinafanya kazi kwa karibu na vikundi mbalimbali ili kuwaleta katika mkondo mkuu wa mchakato wa amani na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa amani, wakidemokrasia na wa kuaminika.